Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Machame Magharibi, chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Diwani wa kata hiyo Martin Munisi, imefanya mkutano wake wa kwanza wa maendeleo na wananchi wa Kijiji cha Kyieri Januari 26,2026.
Akizungumza katika mkutano huo, Diwani Munisi amewashukuru wananchi wa kijiji hicho kwa ushiriki wao mkubwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 uliowawezesha kuchaguliwa kwa Rais, Mbunge na Diwani.
Diwani Munisi ametaja mipango ya maendeleo ya miaka mitano kwa Kijiji cha Kyieri kuwa ni pamoja na kufanyiwa matengenezo makubwa kwa barabara ya Bwani–Kyieri kuboresha barabara za vitongoji vya Maanga, Wongoo na Iwala, pamoja na kujenga maabara katika zahanati ya Kyieri.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kutoa elimu ya bima ya afya kwa wote, sambamba na kushughulikia changamoto za uhaba wa maeneo, upungufu wa nyumba za walimu.
Katika sekta ya kilimo na mifugo, Diwani Munisi amesema serikali inaendelea kutoa chanjo na matibabu mbalimbali kwa mifugo, huku wananchi wakihamasishwa kupima udongo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Hata hivyo ameeleza kuwa katika swala la umwagiliaji, serikali imepanga kuchimba visima vya maji katika maeneo ya Maanga na Iwala, ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji, na kwamba maji hayo yatanufaisha vitongoji vya Kyieri Sinde na Kyieri Ndoo.
Kwa upande wa ulinzi na usalama, Askari Kata Inspekta Glory George John amewapongeza wananchi wa Kyieri kwa ushirikiano wao katika kutoa taarifa za uhalifu, na kuwataka waendelee kutoa ushirikiano ikiwemo ushahidi ili wahalifu wachukuliwe hatua za kisheria.
Diwani Munisi amehitimisha mkutano huo kwa kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao na kuahidi kusimamia utekelezaji wa ahadi zote kama zilivyoainishwa katika ilani ya uchaguzi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai