Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko, amewataka wananchi wilayani humo kuendelea kutunza mazingira kwa kuepuka ukataji holela wa miti na badala yake kujikita katika upandaji wa miti, akisisitiza kuwa mazingira yakitunzwa leo, yatawalinda wananchi hapo baadaye.
Bomboko ametoa wito huo leo Januari 27, 2026, wakati wa zoezi la upandaji miti na usafi wa mazingira lililofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Katika zoezi hilo, Bomboko amesema juhudi za uhifadhi wa mazingira zina mchango mkubwa katika kulinda afya ya binadamu, kuboresha huduma za kijamii na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan katika maeneo ya huduma za afya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Hai, Ng’uni Mganda, ameushukuru uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuona umuhimu wa kuanzisha na kuunga mkono zoezi la upandaji miti katika hospitali hiyo, akibainisha kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha mazingira salama kwa wananchi.
Aidha, Mganda amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi huo wa kuhimiza upandaji miti kote nchini, sambamba na kumtakia heri katika siku yake ya kuzaliwa.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefanikisha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo wilayani Hai, hususan katika sekta ya elimu. Amesema miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa shule mpya na madarasa, ambapo Shule ya Sekondari Hai Day ni miongoni mwa wanufaika wa juhudi hizo.
Zoezi hilo limehitimishwa katika Shule ya Sekondari Hai Day, ambapo Bomboko na uongozi wake walitoa elimu ya maadili na uzalendo kwa wanafunzi, wakisisitiza umuhimu wa kuipenda na kuitumikia nchi kwa kuzingatia nidhamu, maadili mema na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai