Wito umetolewa kwa wapanda pikipiki mkoa wa Kilimanjaro kuvaa kofia ngumu (Helmet) wanapotumia vyombo hivyo vya moto ili kujilinda na kufuata sheria za usalama barabarani.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Usalama barabarani Mkoa wa Kilimanjaro Mrakibu Msaidizi wa Polisi Sauda Mohamed wakati akizungumza na wananchi wa moka huo kupitia Redio Boma Hai FM katika kipindi cha Siku Mpya kinachoruka kila siku saa 11 alfajiri hadi saa 3 kamili asubuhi.
Kamanda huyo wa usalama barabarani amesema kuwa kutakuwa na oparesheni maalumu katika wilaya ya Hai ya kuwakamata waendesha pikipiki wote wasiovaa kofia ngumu na kuwachukulia hatua za kisheria.
Kamanda Sauda amesisitiza kuwa kila mwendesha pikipiki anatakiwa kufuata sheria zote za usalama barabarani kama watumiaji wengine wa vyombo vya moto na kuongeza kuwa ni makosa kwa mwendesha pikipiki kukipita chombo kingine cha moto (kuovateki) kwa upande wa kushoto na kwamba atakayefanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Usalama barabarani Wilaya ya Hai ASP Abdalah Mbaruku amesema kuwa oparesheni hiyo itaanza wiki hii na itakuwa endelevu kuhakikisha kuwa kila mtu anatii sheria bila shuruti kwa kuvaa kofia ngumu na kufuata sheria za usalama barabarani kwa ajili ya usalama wa mali na maisha ya watumia barabara wote.
Mbaruku ameongeza kuwa kosa la kushindwa kuvaa kofia ngumu linawahusu madereva wa pikipiki pamoja na abira wao na kwamba abiria atawajibishwa kwa kutovaa kofia na dereva atakayeshindwa kumpatia abiria wake kofia ngumu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria kwani kila mpanda pikipiki awe dereva au abiria anao wajibu wa kuvaa kofia ngumu.
Aidha watumiaji wote wa barabara wameaswa kujielimisha na kuzifahamu sheria za barabarani pamoja na kuwa waangalifu wanapotumia barabara ili kujihakikishia usalama wao pamoja na watumiaji wengine kwa kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa tatizo la ajali za barabarani.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai