Serikali Kuwakamata Wasiodai na Wasiotoa Risiti za Biashara
Imetumwa: February 17th, 2021
Mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya ameagiza Kamati ya ulinzi na usalama kuhakikisha inashirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuwakamata wafanyabiashara na wateja wanaouza na kununua bidhaa bila kutoa na kudai Risiti za malipo.
Sabaya amesema kuwa watu hao wamekuwa wakisababisha Serikali kukosa mapato stahiki na mamlaka zinazokusanya mapato kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji kodi na maduhuli ya serikali.
Lengai Ole Sabaya ametoa maagizo hayo wakati wa kikao maalum na watendaji wa TRA, Maafisa biashara wa halmashauri pamoja na watendaji wanaohusika na masuala ya fedha wote kwa pamoja wamejadili kuhusu kupandisha mapato ya wilaya ya Hai katika mwaka wa fedha 20021/22.
Sabaya ameagiza hayo baada ya kubainika kuwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kukwepa kulipa kodi na kushindwa kutoa risiti kwa wateja na kuikosesha serikali mapato na kusababisha mamlaka za serikali kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa kodi.
“Naagiza kuanzia Sasa OCD na timu yako kwa kushirikiana na TRA na halmashauri fanyeni operation ya kuwakamata wanaofanya biashara na kushindwa kutoa na kupokea risiti maana ndiyo wanaoikosesha serikali mapato”. Ameagiza Sabaya.
“Utakuta Mtu ananunua mzigo wa mamilioni ya fedha hadai risiti au anafanyia ujanja ujanja wa kupata risiti iliyoambatana na biashara iliyofanyika kamateni weka ndani tupate mapato tujenge barabara, shule, hospitali, tununue dawa na kuleta maendeleo kwa wananchi “Amesema Mkuu wa wilaya Sabaya
Hata hivyo Sabaya ameeleza kwamba hakuna duka lolote lillilofungwa na Mamlaka ya mapato TRA wala akaunti za wafanyabiashara bali wafanya biashara wenyewe wamekuwa wakitoa bidhaa nje ya maduka na kuwapa wafanyabiashara wadogo (machinga) wakauze nje na baadaye kumletea faida na kupewa posho yao ya siku hivyo kusababisha TRA kukosa mapato.
Pamoja na hayo Sabaya amabaini mbinu nyingine inayotumiwa na wafanyabiashara kukwepa kodi za serikali kwa kuuza bidhaa zao kwa mtindo wa kuwakopesha wateja wao na kupokea malipo kwa awamu bila kutoa risiti; mtindo aliouita ‘black market’ na kuziagiza mamlaka husika kufuatilia na kuwakamata watu wanaotumia mtindo huo ili kutambua kama wanalipa kodi stahiki au la.
Naye Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wilayani Hai, Ester Martin Mallya amesema wamekusudia kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 4.6 kwa mwaka wa fedha wa 2020,2021 huku akibainisha kuwa iwapo kutafanyika ufuatiliaji wa kina nakuziba mianya wa kukwepa kodi basi mamlaka hiyo inaweza kukusanya zaidi ya malengo waliyojiwekea.
Amesema katika ukusanyaji wa mapato wanakutana na vikwazo vya wafanya biashara kuuza bidhaa na kuacha kutoa risiti au wakitoa wanatoa ya pesa ndogo jambo ambalo amemuomba mkuu wa wilaya kulisimamia kwa nguvu zote waweze kufikia malengo ya ukusanyaji.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa wilaya Hai; Mwenyekiti wa wafanyabiashara eneo la stand ya Bomang’ombe Anderson Soni ameshukuru kikao cha pamoja na Mamlaka ya Mapato (TRA) na kupata mafunzo kwani wamekua wakiogopa kukutana nao na kufanya mashairiano ya juu ya kiendesha biashara.