Uwekaji wa taa katika soko la Gezaulole lililopo wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wafanyabiashara, kwani utawawezesha kufanya shughuli zao katika mazingira salama na rafiki zaidi.
Kauli hiyo imetolewa na Diwani wa Kata ya Bomang’ombe Evod Njau, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa robo ya pili ya mwaka, kuanzia Oktoba hadi Desemba, katika mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika Februari 6, 2026 katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai.
Hata hivyo Njau amesema kwa sasa wafanyabiashara katika soko hilo wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mwanga, hali inayowalazimu kufunga biashara zao mapema na hivyo kuwanyima fursa ya kuongeza kipato chao cha kila siku.
Aidha, akizungumzia suala la usafi wa mazingira katika kata ya Bomang’ombe Njau amesema uwepo wa gari moja pekee la kukusanya taka umekuwa kikwazo kwa mkandarasi, hali inayosababisha taka kutochukuliwa kwa wakati na wakati mwingine kuchukuliwa mara moja tu kwa mwezi.
Kutokana na hali hiyo, Diwani Njau ameiomba Halmashauri ya wilaya ya Hai kuangalia uwezekano wa kununua gari lingine la kukusanya taka, ili kuboresha usafi wa mazingira na kuendelea kulinda afya ya wananchi wa kata hiyo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai