Vijana wametakiwa kutumia changamoto zilizopo kwenye jamii na kuzitumia kama fursa ya kujinufaisha kiuchumi kwa kutafuta utatuzi wa changamoto hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Vijana Mkoa wa Kilimanjaro Irine Kiata kwenye maadhimisho ya wiki ya vijana na kumbukizi ya Baba wa Taifa katika viwanja vya halmashauri Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.
Ametoa mfano wa changamoto ya uwepo wa taka inaweza kugeuzwa fursa kwa kuanzisha shughuli za kuzoa taka kwa malipo kutoka kwa wananchi watakaofaidi huduma hiyo na kufanya vijana kupata ajira na kujiongezea kipato.
“Vitabu vya maandiko vinatuambia kuwa sisi vijana tuna nguvu; na fahari yetu ni nguvu. Napenda kuwasihi vijana; mwendelee kufanya kazi kwa bidii na kwa kupitia nguvu zetu tutafanikiwa”
“Niombe pia mashirika tunayoshirikiana nayo kuanza kubadili mipango yao katika kuhudumia vijana kwa kuanza kuwapa elimu wanayostahili badala ya kusubiri waharibikiwe na kuanza kushighulikia matokeo. Tuwape vijana elimu ya namna bora ya kufanya mambo yao kwa ufanisi bora zaidi” Ameongeza Kiata.
Aidha Kiata ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa kutambua umuhimu wa vijana na kuwapa nafasi ya kushiriki kwenye maadhimisho ya siku yao kwa kuonesha vipawa vyao kwenye ubunifu, Sanaa, biashara na nyingine pamoja na kuwapa nafasi ya kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa vijana wenzao waliofanikiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo ameahidi kusimamia utekelezaji wa kazi za Serikali katika halmashauri yake ikiwemo shughuli za Kitaifa kuadhimishwa kwa wakati wake kama ilivyo kumbukizi ya Kifo cha Mwalimu Nyerere.
Sintoo amesema kuwa halmashauri ya Hai itaendelea kutoa usaidizi kwa vijana ikiwemo kuwapatia mikopo isiyo na riba pamoja na kuwakutanisha na elimu ya ujasiriamali ili waanzishe miradi yenye tija itakayowaongezea kipato na kuweza kutengeneza ajira kwa vijana wengine.
Amesema halmashauri yake inatekeleza hayo ikiwa ni namna ya kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo katika kupambana na maadui watatu wa ujinga, umasikini na maradhi.
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi; Afisa Vijana Wilaya ya Hai Lucila Chima amesema Serikali kwa upande wake imeweka sera na mipango madhubuti ya kuwaendeleza vijana katika kujiajiri, kuanzisha na kuendeleza viwanda, kudumisha amani, usawa na kuleta maendeleo kwa kutumia rasilimali na fursa zilizopo kwenye maeneo yao.
Chima amewakumbusha vijana wenzake kutumia fursa za mazingira yaliyowekwa na Serikali ili kujitengenezea shughuli za kuwaingizia kipato na kuwasaidia kujikwamua na umasikini ikiwa ni pamoja na kutengeneza ajira kwa vijana wenzao katika sekta za kilimo, usafirishaji, Sanaa na ubunifu.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai