Mkuu wa Wilaya ya Hai Juma Irando amewahimiza wananchi katika wilaya hiyo kujitokeza kupata chanjo kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 unaohatarisha maisha ya watu duniani kote.
Irando ametoa kauli hoyo wakati wa uzinduzi wa chanjo ya corona aliyoizindua katika Hospitali ya Wilaya ya Hai siku ya Jumanne 03/08/2021 kwa kuongoza kuchoma chanjo hiyo akifuatiwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.
Amewasisitiza wananchi kuacha kufuata ushauri wa wapotoshaji wanaotoa kwenye mitandao ya kijamii kwani wana malengo ya kuwaongezea wananchi hofu kwa kuwapa habari za uongo zisizothibitishwa; badala yake amewataka wananchi kusikiliza ushauri wa wataalamu wa afya wanaoaminiwa na serikali ikiwemo Wizara ya Afya na wataalamu wake.
Aidha Irando amemwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuwapa uelewa sahihi kuhusu chanjo ya corona na kuwaondolea imani potofu walizonazo ili watu wengi waweze kujitokeza kupata chanjo na hatimaye wilaya ya Hai kuendelea kuwa salama huku akisisitiza kuwa kupata chanjo ni jambo la hiyari.
Naye Adinani Msangi; mmoja wa wananchi waliojitokeza kupata chanjo hiyo amesema kuwa watu wengi wapo tayari kupata chanjo hiyo lakini bado wameathiriwa na hofu wanayojazwa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii.
“Wapo jamaa zangu wanasema wapo tayari kuchanja lakini wanaendelea kujishauri lakini kila mtu anatakiwa kujitambua na kufanya maamuzi ya kujikinga na kuwakinga wengine” amesema Msangi.
Zoezi la kutoa chanjo dhidi ya UVIKO 19 linaendelea katika Hospitali ya Wilaya ya Hai ambapo wananchi wanaendelea kupatiwa chanjo hiyo ikiwa ni juhudi za Serikali kuwakinga wananchi wake dhidi ya madhara ya ugonjwa wa Corona ikiwemo kupunguza wagonjwa wanaohitaji kuwekewa hewa ya oksijeni na kupunguza vifo.