Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengei Ole Sabaya amesitisha mpango wa kuwasimamisha masomo wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Moshi kilichopo kwenye Kata ya Bondeni wilayani Hai.
Akizungumza na wanafunzi na uongozi wa chuo hicho Sabaya amemtaka Mkuu wa Chuo hicho kusitisha zoezi la kuwafukuza masomo wanafunzi hao au kujaribu kuwalipisha tena ada ambayo walishalipa.
Amesema kumetokea upotevu wa fedha za chuo zilizolipwa na wanafunzi lakini bado hazionekani kwenye akaunti ya chuo kutokana na muundo wa uongozi kuwa na kasoro na kwamba upotevu huo hauwahusu wanafunzi ambao wameshatimiza wajibu wao wa kulipa fedha hizo.
“Nakuelekeza Mkuu wa Chuo; usifukuze mwanachuo hata mmoja na wala wasilipe fedha mara ya pili kwa sababu muundo wa uongozi wa chuo chenu una kasoro na ndio maana kumetokea upotevu” amesema.
Naye Mkuu wa Chuo hicho Fredrick Akyoo amemthibitishia Mkuu wa Wilaya kuhusu upotevu wa fedha hizo akibainisha kuwa mnamo Septemba 2018 wanafunzi walimpatia fedha Mhasibu wa chuo hicho zaidi ya shilingi milioni 6 zikiwa ni malipo ya ada ya masomo.
Aidha Akyoo amemweleza Mkuu wa Wilaya kuwa mhasibu huyo ameweza kutengeneza stakabadhi 380 za malipo hewa alizowagawia wanafunzi waliolipia fedha kwake ambazo kati ya shilingi millioni 60.2 ni shilingi millioni 5 tu ndizo zinazoonekana kuingia kwenye akaunti ya chuo.
Anasema wanafunzi walilipa fedha hizo mkononi kwa mhasibu na sio kwenye akaunti ya chuo kwa makubaliano ya kupatiwa risiti zikisha kuwa tayari hivyo kufanya iwe rahisi fedha hizo kupelekwa kwenye matumizi tofauti na ya chuoni hapo.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho walioathiriwa na mkasa huo wamesema kuwa wamekuwa wakipeleka malipo ya ada kwa mhasibu wa chuoni hapo ambaye amekuwa akiwapatia stakabadhi za malipo hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Hai ameingilia sakata hili baada ya wanafunzikutaka kuandamana hadi ofisini kwake kumuomba awasaidie kupata haki yao ikiwemo kutorudishwa nyumbani lakini pia kutolipa upya malipo ya ada.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai