Diwani wa Kata ya Muungano Edmund Rutaraka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai amechangia mifuko 40 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na choo kwenye shule zilizo kwenye kata yake.
Rutaraka ametoa mifuko 20 ya saruji kujenga chumba kimoja cha darasa kwenye Shule ya Masingi Kambi ya Raha na mifuko 20 katika Shule ya Sekondari Hai ambayo itatumika kujenga vyoo vya wanafunzi ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma bila usumbufu.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kambi ya Raha Dorothea Mboya amemshukuru Diwani kwa mchango wake kuimarisha utoaji wa elimu kwenye shule hiyo akibainisha kuwa shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa vyumba 14 vya madarasa ambapo pia darasa moja linalazimika kutumiwa na wanafunzi zaidi ya 100.
Mwalimu Mboya amesema kuwa msaada huo utawasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuongeza ufanisi huku akiomba mchango kutoka kwa wadau wengine ili kuwasaidia kupunguza na hatimaye kumaliza tatizo la uhaba wa madarasa.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Hai Mwalimu Alex Warioba amesema wanamshukuru Diwani huyo kwa namna anavyojitoa kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto wanazokutana nazo na kwamba amekuwa mtu wa karibu kusaidia shule hiyo kila panapotokea uhitaji.
Akishukuru kwa niaba ya wanafunzi wenzake; mwanafunzi Stephano Kabugumila wa Kidato cha Tano amesema miundombinu mizuri ni mchango mkubwa kwa wanafunzi kufanya vizuri kwenye masomo na kuahidi kuwa watatunza miundombinu ya shule ili iweze kuwanufaisha wanafunzi wengi zaidi.
Diwani Rutaraka ameendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwapatia elimu watoto wote wenye umri wa kwenda shule kwa kushirikiana na jamii kuimarisha upatikanaji wa elimu kwa kuboresha miundombinu na huduma nyingine za kielimu.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai