Wilaya ya Hai inaendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha kiwango cha ufaulu kwenye mitihani ya kitaifa kwa kuimarisha sekta ya elimu katika wilaya hiyo.
Kwa miaka minne mfululizo wilaya hiyo imefanikiwa kufanya vizuri kwenye mitihani ya Kitaifa ngazi ya elimu ya msingi na sekondari kwa upande wa kidato cha nne pamoja na kidato cha sita.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Yohana Sintoo wakati akizungumza katika harambee ya kuchangia fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara na ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya sekondari Mailisita iliyopo Kata ya Mnadani wilayani humo.
“Katika wilaya ya Hai elimu imeendelea kufanya vizuri sana, tumeendelea kufanya vizuri katika Taifa hili ambapo tumefanikiwa kuwa katika Halmashauri kumi bora kwa mfululizo wa miaka minne hadi leo” amesema Sintoo.
Akizungumzia mipango ya Serikali kuimarisha elimu; Sintoo amesema kuwa Halmashauri imepokea zaidi ya milioni 900 kwa ajili ya kukarabati shule ya sekondari ya wasichana Machame, huku zaidi ya milioni 800 zikitolewa kukarabati shule ya sekondari Lyamungo na shilingi milioni 64 zikipelekwa katika shule ya sekondari Longoi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu.
Awali akisoma risala mbele ya Mgeni Rasmi; Mkuu wa Shule ya Sekondari Mailisita; Josina Misago amesema shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa hali inayopelekea wanafunzi zaidi ya sabini kusoma katika chumba kimoja cha darasa huku wengine wakilazimika kwenda kusoma katika chumba cha maabara ambacho hakijakamilika ujenzi wake.
“Changamoto ni uhaba wa madarasa ukilinganisha kwamba darasa linakaa wanafunzi 40, sisi kwetu wanafika 50 hadi 70 kwahiyo hiyo inatupa adha kubwa hasa katika usimamiaji wa taaluma darasani mwalimu inakuwa nivigumu kufuatilia watoto.”amesema
Kuhusu maabara amesema kuwa ukosefu wake umesababisha kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa masomo ya sayansi huku wanafunzi wengi wakishindwa kuchagua mchepuo wa Sayansi hivyo ameiomba serikali na wadau wa elimu nchini kujitokeza kuchangia kukamilisha ujenzi wa maabara pamoja na madarasa ili kuondoa adha hiyo.
Hata hivyo katika harambee hiyo ambayo iliendehswa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Yohana Sintoo na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa elimu Kilimanjaro iliwafanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Milioni 65 kati ya milioni 115 zilizokadiriwa kukusanywa huku ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji ikichangia Milioni 25.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai