IMEELEZWA kuwa tatizo la utapia mlo limekuwa likiathiri jamii ya kitanzania hasa watoto ambao ni tegemeo kubwa kwa taifa na uboreshwaji wa hali ya lishe nchini jambo ambalo linatakiwa kutolewa elimu juu ya kupambana na hali hiyo.
Kufuatia hali hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Yohana Sintoo amesema kuwa ili kukabiliana na tatizo hilo lazima kamati lishe ya wilaya kujikita katika kuelimisha kuhusu lishe bora kwa watoto ili kuondokana na tatizo la utapiamlo.
Akizungumza katika uzinduzi wa kamati ya Lishe ya Wilaya; Sintoo amesema kuwa ni lazima kamati hizo kuwa na mikakati ya kutoa elimu bora ya namna ya kukabiliana na utapiamlo ambao husababishwa na lishe duni.
Amesema tatizo la lishe duni limekuwa likiathiri ukuaji wa maendeleo ya mtoto kimwili na kiakili hali hiyo hufifisha mchango wake katika ukuaji wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai Dkt. Irene Haule amesema kuwa mafunzo ya kuboresha huduma za lishe yatasaidia katika kuhakikisha kunakuwepo mabadiliko chanya katika makuzi ya mtoto ambaye ni tegemeo kwa taifa na jamii kwa ujumla.
Dkt. Haule amesema kuwa kati ya watoto 46,000 walio chini ya umri wa miaka 5 waliofika kwenye vituo vya kutolea huduma mwaka 2017 waliogundulika na utapiamlo ni 217 tu.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Wilaya Hai, Silivania Kullaya amesema licha ya kuwepo kwa tatizo la utapiamlo kumekuwepo pia magonjwa wa Kusendeka ambao husababishwa na mitindo mibaya ya maisha kama vile ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi, kutokufanya mazoezi, kutokupima afya, unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara.
Amesema kuwa ili kukabiliana ugonjwa huo lazima jamii ielimishwe kuhusu ulaji sahihi na mfumo mzuri wa maisha kwa kufuata taratibu za lishe hali itakayowezesha kuwa na jamii yenye Afya njema.
Akihitimisha uzinduzi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Hai, Julias Kakyama ameitaka kamati hiyo kuzingatia mafunzo waliyopewa ambayo yamejadili mustakabali wa afya ya wakazi wa Wilaya ya Hai.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai