Maliasili Washauriwa Kuboresha Fidia Madhara Yanayosababishwa na Wanyamapori
Imetumwa: May 12th, 2021
Katibu Tawala Wilaya ya Hai Upendo Wella ameiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia viwango wanavyopatiwa wahanga wa matukio ya ajali zinazohusisha wananchi na wanyama pori.
Ameishauri Wizara hiyo kuangalia namna ya kuboresha kiwango kwa kuzingatia hali halisi ya maisha pamoja na thamani ya uharibifu au madhara yaliyotokea.
Wella ametoa ombi hilo kwa Wizara wakati akishuhudia makabidhiano ya fedha za kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi 4 wa Wilaya ya Hai ambao wamepata madhara na hasara vilivyosababishwa na wanyama pori.
Akiongoza wataalamu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Afisa Wanyamapori Mkuu Nassoro Wawa amesema wamekuja kuwapa sehemu ya fidia wananchi 2 ambao wengine wamepata majeraha yasiyo ya kudumu na wengine 2 ambao mazao yao yaliharibiwa na wanyama.
Wawa amesema kanuni zinaelekeza kutoa kifuta machozi kwa wananchi ambao wamepata majeraha ambapo shilingi 200,000 hutolewa kwa aliyepata majeraha yasiyo ya kudumu na shilingi 500,000 kwa majeraha au kilema cha kudumu huku wakitoa kifuta jasho cha shilingi 100,000 ekari kwa wale ambao mazao yao yameharibiwa na wanyama pori na shilingi 1,000,000 kwa mwananchi aliyeuwawa na wanyama.
Aidha Afisa Wanyamapori anayehudumu katika Wilaya za Hai na Siha Lyimo amesema matukio ya wanyamapori kujeruhi au kuharibu mazao yanatokana na wananchi kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo ya mapito ya wanyama pori au wanyama kutafuta malisho hasa wakati wa kiangazi huku akisisitiza kuwa fidia inalipwa kwa wananchi waliothibitikshwa kuwa nje ya maeneo ya hifadhi za wanyama pori.
Kwa upande wake Charles Palanjo mkulima wa Kijiji cha Sanya Station ambaye sehemu ya shamba lake liliharibiwa na mnyama wa porini (nyati) ameishukuru Serikali na maafisa maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa ushirikiano waliompa hadi na kumwelimisha taratibu za kufuata hadi kufikia kulipwa kifuta jasho.
Amewaasa wananchi wengine kuacha kulalamika wanapokutana na uharibifu bali wawasiliane na mamlaka husika ngazi ya wilaya kwa ajili ya kutoa taarifa ili taratibu za kisheria zifuatwe.
Serikali imeendelea kusisitiza kufuata taratibu hasa wananchi kuweka makazi na kufanya shughuli za maendeleo mbali na maeneo ya wanyamapori ili kuepusha madhara lakini pia kuwahimiza wananchi wote kuwa sehemu ya kuhifadhi na kulinda maliasili zilizopo kwa manufaa ya Taifa.