Milioni 72 Kutatua Kero ya Maji Kata ya Muungano Wilayani Hai
Imetumwa: March 15th, 2021
Zaidi ya shilingi milioni 72 zimetengwa kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji ikiwa ni kuibadilisha miundombinu ya bomba kubwa la maji kutokea Hai day hadi Kanisa Katoliki kingereka katika kata ya Muungano wilayani Hai ili wananchi ambao hawapati huduma ya maji waweze kupata huduma hiyo hasa wakati wa mgao.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na diwani wa kata ya Muungano Edmund Rutaraka wakati akisikiliza kero za wananchi wa kata hiyo ambapo amesema kuwa mbali na kero ya maji katika maeneo ya kata yake kuwa ni ya muda mrefu tayari RUWASA wamekwisha pokea milioni 72 ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Rutaraka amesema kuwa bado serikali inaendelea na kutatua kero mbali mbali kwa wananchi wake huku pia akiishukuru pia serikali kwa kuanza ujenzi wa barabara ya dorcas kwa kiwango cha lami ambapo ilikuwa ni changamoto kubwa kwa wasafiri.
Kata ya Muungano inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ukosefu wa baadhi ya vyumba vya madarasa katika Shule ya msingi Kambi ya Raha ambapo tayari vikao vimeanza kufanyika na kiasi cha milioni 7.5 zitaitajika kunyanyua boma amabalo serikali itamalizia kwa 12.
Katika kutatua changamoto hizo Rutaraka amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kusukuma gurudumu la maendeleo huku akiahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo katika kipindi kifupi jambo litakalosaidia wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji na kimaendeleo bila kuwepo kwa vikwazo hivyo.