Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Yohana Sintoo amewataka watumishi wa umma kwenye halmashauri hiyo kutekeleza wajibu wao kwa weledi na kuzingatia kutoa huduma bora kwa wananchi kwenye maeneo yao.
Sintoo ametoa rai hiyo mapema leo katika ukumbi wa halmashauri hiyo kwenye kikao kazi cha siku moja cha watendaji wa serikali wa kada mbalimbali kwenye ngazi ya kata na vijiji kilichokuwa na lengo la kuwakubusha utaakelezaji wa majukumu yao na kuboresha huduma kwa wananchi.
“Baadhi ya watendaji wamekuwa na tabia za kukwepa majukumu yako , ya kutatua kero za wananchi na kugeuka kuwa sehemu ya migogoro kwa kuwapendelea baadhi ya watu ”amesema Sintoo.
“Watendaji wa kata hakikisheni kuwa mnasimamia watendaji wa vijiji pamoja na wataalamu wote waliopo kwenye maeneo yenu ya utawala ili wawajibike na kuhudumia wananchi kwa kiwango kinachostahili ikiwemo kuondoa migogoro inayojitokeza kwenye jamii” amesisitiza Sintoo.
“Wapo watendaji miongoni mwenu wamekuwa na tabia za kufungua ofisi asubuhi na kuondoka kwenda kwenye shughuli zao za binafsi na kuwaacha wananchi wakipata shida pindi wanapohitaji huduma, tabia hii sitaivumilia na wala sitasita kumchukulia hatua za kinidhamu yeyote atakayebainika ”ameongeza.
Akizungumzia suala la baadhi ya wenyeviti wa mitaa na vijiji kuingiza siasa katika shughuli za kimaendeleo, Sintoo amesema tabia hii imechangia kuchelewesha upatikanaji wa huduma za kijamii kutokana na kuwagawa wananchi kwa itikadi za kisiasa
“Niwaombe wenyeviti kuepuka kuingiza siasa kwenye utekelezaji wa shughuli za maendeleo na mfahamu kuwa utekelezaji wa kazi za serikali hauzingatii upendeleo wa aina yoyote au itikadi ya chama chochote kwani maendeleo hayana chama” ameongeza Sintoo
Kwa upande wake mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Boniface Kalokona amewataka watumishi kuacha tabia za kufanya kazi kwa woga ili kukwepa lawama na badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo ambazo hazipendelei wala kumuonea mtu yeyote bali zinatoa haki sawa kwa wote.
Naye mratibu elimu kata ya Weruweru Angelika Kesi amesema kikao hicho kimewakumbusha majukumu yao pamoja na kupata njia za kuweza kutatua changamoto zinazijitokeza kwenye maeneo yao hali ambayo itasaidia kuboresha huduma kwa wananchi.
Katika kikao kazi hicho kilichowahusisha watendaji wa kata, watendaji wa vijiji, waratibu elimu kata, maafisa maendeleo ya jamii kata pamoja na wakuu wa idara zao; kila mtaalamu alipata nafasi ya kuzungumzia changamoto moja kwenye eneo lake la kazi na namna ilivyotatuliwa lengo likiwa kutambua namna watendaji hao wanavyowatumikia wananchi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai