Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hai Dionis Myinga amezindua rasmi zoezi la mfumo wa anwani za makazi wilayani humo na kuwaagiza watendaji wote kuanza utekelezaji mara moja ili kuhakikisha zoezi hilo linakamilika mapema kabla ya mwezi Mei mwaka huu.
Myinga ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo na kuwataka kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufikia lengo lililowekwa na serikali kuhakikisha kila eneo linakuwa na anwani za makazi.
“Naomba watendaji wote mkafanye kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha kwamba hili zoezi linatekelezwa na linakamilika mapema kabla ya mwezi wa tano ambao ndiyo muda uliopangwa na Serikali, kwani tukimaliza mapema tutapata muda wa kurekebisha vipengele vichache ambavyo pengine vitakuwa havijakaa sawa” amesema Mkurugenzi Myinga
Aidha Mkurugenzi huyo amewataka wananchi kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kushiriki ipasavyo kwenye utekelezaji wa zoezi hilo kwa kuwa manufaa yake ni makubwa ikiwa ni pamoja na kurahisisha upatikanaji, utoaji na ufikishaji wa huduma katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake Afisa Tehama kutoka halmashauri hiyo Bw. Arnold Malisa ameeleza kuwa ni wakati sasa kwa maeneo yote kuingizwa katika mfumo wa anwani za makazi ili kuondokana na mfumo usiodhahiri wa kuelezea mahali kwa njia ya uwakilishaji ambayo inatajwa kuleta utata.
Serikali inatekeleza mpango wa Anwani za makazi na postikodi kwa kila kata ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya taifa ya posta ya mwaka 2003, makubaliano ya kimataifa (Pan African Postal Union PAPU), Universal Postal Union pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya 2020-2025.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai