Katika ziara yake ya kukagua miradi ya serikali wilayani Hai, Mkuu wa Wilaya, Mheshimiwa Hassan Bomboko, ameguswa na juhudi za Anna Boniface, mwanamke anayefanya kazi katika ujenzi wa shule, ambaye ameonyesha kuwa kazi si kwa ajili ya wanaume pekee.
Anna Boniface amesema kuwa mwanzoni watu walishangazwa na uamuzi wake wa kufanya kazi hiyo, lakini kwa sasa wameshaizoea, ikiwemo familia yake.
"Nina miaka mitano nikifanya kazi hii, na mume wangu naye amenizoea. Nawaambia wasichana wenzangu wasichague kazi. Ni kweli kuna kazi ngumu, lakini sio zote ni za wanaume pekee. Kama mimi nimeweza, basi na wengine wanaweza pia," amesema kwa kujiamini.
Mkuu wa Wilaya, Mheshimiwa Bomboko, amemsifu Anna Boniface kama mfano wa kuigwa kwa vijana, hasa wa kike, akisema kuwa bidii yake inaonyesha umuhimu wa kujituma bila kujali jinsia.
"Tunataka kuona watu wengi zaidi wakifanya kazi na kushiriki katika miradi ya maendeleo. Kazi sio ya jinsia fulani, bali ni kwa yeyote mwenye nia na uwezo," amesema.
Anna Boniface pia ametoa wito kwa vijana waache uvivu na kutumia fursa zilizopo badala ya kupoteza muda vijiweni.
"Vijana siku hizi wamekuwa wavivu kufanya kazi. Nataka kuwaambia—kazi ipo, kinachohitajika ni juhudi na moyo wa kujituma," amesema.
Pia amepongeza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kwa miradi ya maendeleo, hususan ujenzi wa shule, akisema kuwa miradi hiyo imetoa ajira kwa wananchi wengi.
"Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa miradi hii, maana bila miradi hii, ajira zingekuwa chache sana. Tunaomba aendelee kutufikiria kwani anatupenda, na tumeona hilo kwa kazi kubwa inayofanyika," ameongeza.
Ziara ya Mheshimiwa Bomboko imeendelea kuibua simulizi za mafanikio kama haya, zikithibitisha kuwa kupitia miradi ya serikali, wananchi wengi wanapata fursa za kujiajiri na kuendesha maisha yao kwa heshima na bidii.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai