Mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya ameunda kamati maalumu ya kushughulikia madai ya posho za waalimu waliohamishwa vituo vya kazi kutoka shule za sekondari kwenda shule za msingi.
Akizungumza kwenye kikao na watumishi hao wakiwemo walimu kutoka shule za msingi na sekondari kwenye ukumbi wa KKKT Hai mjini kikiwa na lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zao ikiwemo kupandishwa madaraja.
Sabaya amesema kamati hiyo itaongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo pamoja na wajumbe kutoka ofisi ya mkurugenzi huku akiwaongezea wajumbe wawili ambao ni afisa TAKUKURU na afisa wa usalama wa Taifa itakayokuwa na kazi ya kuhakiki vigezo vilivyotumika kuwalipa posho baadhi ya waalimu huku wengine wakiachwa na kushughulikia madai ya posho hizo.
Aidha amewahakikishia waalimu hao kuwa serikali wilayani Hai ipo pamoja nao hasa katika kushughulikia matatizo na kero mbalimbali wanazokumbana nazo na kuwataka kuendelea kutekeleza majukumu yao bila wasiwasi.
Awali akitoa utangulizi wa kikao hicho; Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amewataka watumishi waliohudhuria kikao hicho kusema yale yote yanayowatatiza na kuwasababisha wasifanye kazi kwa amani ili yatatuliwe na kuboresha utekelezaji wa kazi zao.
“Nichukue nafasi hii mimi kama mwajiri; kuwaomba watumishi wenzangu kutumia kikao hiki kusema yale yote yanayowakwaza ili tuyatatue kwa pamoja kwa ajili ya kuboresha utendaji wa kazi zetu”. Ameongeza Sintoo.
Akichangia mawazo kwenye kikao hicho; diwani wa kata ya Machame Magharibi Martin Munisi amesema walimu ni kada ya heshima sana kutokana na majukumu yao ya kuandaa vizazi vijavyo vya jamii hivyo kutoa rai kwa mamlaka zinazohusika na maslahi ya walimu kuwatendea haki ili kuwafanya watekeleze majukumu yao kwa ufanisi bila manung’uniko.
Mwaka 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Hai iliwahamisha walimu 277 kutoka shule za sekondari ili kusaidia kupunguza upungufu wa walimu kwenye shule za msingi zoezi ambalo lilikamilika na kuacha mapungufu kadhaa ikiwemo malipo ya posho kwa baadhi ya walimu waliohamishwa.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai