Chama cha Msalaba Mwekundu (RED CROS) Mkoa wa Kilimanjaro kimekabidhi msaada wa Magodoro 20, blanket 20 kwa wahanga wa mafuriko yaliyotokea hivi karibuni Katika kijiji cha Ntakuja Kata ya Kia wilayani Hai.
Mafuriko hayo yalisababishwa na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Aprili 23 mwaka huu na kufanya kaya zipatazo 20 kukosa makazi kutokana na nyumba zao kubomolewa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo; Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amesema baada ya kutokea kwa maafa hayo kamati ya maafa wilaya ilikagua uharibifu uliotokea na kubaini kaya hizo 20 kukosa makazi hivyo Halmashauri ikaona ni vyema kupokea misaada kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuzisaidia kaya hizo.
Pia amesema kuwa Halmashauri hiyo inaendelea kupokea michango mbalimbali na kuifikisha kwa wahanga wa mafuriko hayo huku akiwataka viongozi wa eneo hilo pamoja na wananchi kuepuka udanganyifu pamoja na kuwa waaminifu kwenye misaada hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Msalaba Mwekundu Mkoa wa Kilimanjaro Ester Maleko amesema kuwa wamekuwa wakigusa na kusaidia maisha ya mwanadamu na kupunguza madhara yanayowapata wananchi ikiwemo mafuriko katika makazi na kwamba bado wataendelea kushirikiana na halmashauri kuwasaidia wananchi hao wakati wowote.
Nao baadhi ya wananchi waliopata msaada huo wameishukuru serikali na chama hicho kwa kuona umuhimu wa kuwafikishia msaada huo kwani tangu kutokea kwa maafa hayo wamekuwa wakipata wakati mgumu wa kuishi huku ikiwalazimu wengine kuishi kwa majirani.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai