Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira amepongeza ushiriki wa wananchi kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Hai.
“watu wa Hai wanatia moyo sana, nimeona miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa nguvu ya wananchi, ni hali nzuri na inafurahisha sana na inatia moyo ”
Ameyasema hayo kwenye mji mdogo wa Bomang’ombe wakati wa ziara yake ya kujitambulisha wilayani humo ambapo amekagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Hai ikishirikiana na wadau mbalimbali na kwa kiasi kikubwa imehusisha nguvu ya wananchi kwenye maeneo husika.
Pamoja na pongezi hizo, Mghwira amewataka viongozi wote kuanzia Mkuu wa Wilaya, Madiwani na viongozi wengine kushiriki katika kuhamasisha wananchi kuendelea kujitokeza kuibua na kuchangia miradi ya maendeleo huku akiwapa changamoto Mkurugenzi na wataalamu wake kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha inafanikiwa kwa viwango vinavyohitajika.
“Kinachobaki ni usmimamizi wa wataalamu na mameneja wanaohusika, wananchi wako tayari kuchangia na kufanya mambo yatokee. Hii inatia moyo hata serikali kuongeza nguvu kwa sehemu inayobakia pale inapohitajika kuongeza nguvu kwenye mambo yaliyoibuliwa na wananchi”
Mghwira amefanya ziara ya kujitambulisha katika wilaya ya Hai ambapo amekagua miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo la upasuaji, ujenzi wa jengo la duka la dawa la bima unaogharimu milioni 44.9 unaotekelezwa kwa kushirikiana na Mfuko wa Bima ya Afya yote ikiwa ni kwenye hospitali ya wilaya hiyo.
Pia alikagua ujenzi wa daraja la Mto Sanya wenye thamani ya sh. 114,200,600 na vyumba vya madarasa kwenye shule za Msingi Gezaulole na Bomani ambazo zimejengwa na wananchi hadi kufikia kiwango cha kupaua.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai