Serikali imedhamiria kuongeza idadi ya kaya masikini zitakazopatiwa huduma kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kuwezesha kaya masikini kuondokana na hali hiyo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Ummana Utawala Bora Capt. Mstaafu George Mkuchika akiwa kwenye ziara ya kikazi katika Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro.
Captain Mstaafu Mkuchika amesema kuwa mpaka sasa Serikali ya awamu ya tano imefikia asilimia 70 ya kaya masikini zinazonufaika na huduma ya fedha ambazo zimekuwa zikitolewa kwa ajili ya kupunguza makali ya maisha.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kaya zote ambazo hazina uwezo wa kujikimu kimaisha zinawezeshwa ili ziweze kujitegemea.
Hata hivyo, Waziri huyo amewataka wanafamilia wa mpango huo kuungana na Serikali na kuanzisha miradi midogomidogo itakayowasaidia kujiongezea kipato.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji, Mratibu wa TASAF Wilaya ya Hai Herick Marisham amesema kuwa jumla ya kaya 4051 ziliibuliwa katika hatua za awali lakini mpaka sasa kaya 3901 ndizo zilizoweza kukidhi vigezo na kuweza kuingia katika mpango.
Marisham amesema katika kaya hizo zilizoibuliwa, Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 2.7 tangu kuanza kutekelezwa kwa mpango Juni 2015 hadi Agosti 2018.
Akizungumzia katika mkutano huo Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Hai, Kumotola Kumotola amemwomba Waziri huyo kuongeza idadi ya watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili waweze kwenda na kasi ya mapambano ya rushwa.
Kwa upande wao wanufaika wa mpango huo, wamesema fedha hizo zimewasaidia kuboresha maisha pamoja na familia na kuondokana na hali tegemezi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai