SERIKALI ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imetangaza nia ya kulirejesha eneo lenye ukubwa wa ekari mia moja kumi na mbili lililokuwa linamilikiwa na Chama cha Lyamungo AMMCOS baada ya kuwa katika mgogoro kwa zaidi ya miaka kumi na sita.
Shamba hilo lililopo katika Kata ya Machamae Mashariki wilayani Hai linadaiwa kumilikiwa na Chama hicho baada ya kununua kotoka kwa Mgiriki Philip Filios ambapo liliuzwa kwa njia mnada wa hadhara.
Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amesema uamuzi huo wa Serikali umekuja baada ya kudaiwa kuwa eneo hilo limepokwa na Chama Kikuu cha Ushirikia mkoani hapa (KNCU)kinyume na taratibu.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara, Ole Sabaya amesema, uamuzi huo umefikiwa baada ya wananchi kuzuiwa kwa muda mrefu kutumia eneo hilo lililokuwa linamikiwa na wanachama wa chama hicho.
“Shamba hili naamini ni mali yenu ambalo mlinunua kwa fedha za mkopo kiasi cha shilingi laki mbili na mlianza kwa kulipa deni hilo mara ya kwanza 158,000 awamu ya pili mlilipa kiasi 11,460 na awamu ya tatu mkalipa kiasi 8,600 ” amesema.
“Naamini kabisa mlilipa deni kwa asilimia 90 kwani deli lililokuwa limebaki lilikuwa ni kiasi cha shilingi 12,000 ambazo nazo mlilipa kupitia KNCU kwa kukatwa fedha wakati wa kuuza kahawa ”amesema Ole Sabaya.
Amewataka wanachama hao kuhakikisha kuwa wanafanya shughuli za uzalishaji katika shamba hilo pamoja na kujengwa shule kwa ajili ya kuhudumia watoto ili kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu.
Kwa upande wake mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Wakili Henglibert Bonifas amepitia nyaraka zote zilizowasilishwa katika ofisi za halmashauri na kwamba ofisi yake imejidhirisha kuwa kuna ujanja umefanywa na KNCU ili kuwadhulumu wanachama hao shamba hilo.
“Nimejidhirisha kuwa Lyamungo walirejesha fedha za mkopo waliochukua kwa ajili ya kununua shamba hilo kutokana na mkataba waliongia na KNCU wakati wakinunua shamba hilo kutoka kwa mgiriki na kurejesha fedha hizo”
“Baada ya kurejesha fedha hizo na zilizosalia waliingia katika mkataba na KNCU wa kuwakata fedha kwenye mauzo ya kahawa lakini KNCU walishindwa kutoa hesabu za fedha ambazo walikata kwenye mauzo hayo” alifafanua mwanasheria huyo
Awali akisoma taarifa; Mwenyekiti wa AMCOS hiyo, Gabriel Ulomi amesema licha ya jitihada mbalimbali zilizokuwa zikifanywa na viongozi wa serikali kwa ajili ya kumaliza mgogoro uliopo wa KNCU, kutokana na Chama hicho cha ushirika kung’ang’ania shamba hilo ni mali yao pasipokuonyesha uhalali wa umiliki.
Alifafanua kuwa Chama hicho kilikuwa na mipango mbalimbali ya uwekezaji nje ya zao la kahawa kwa ajili ya kukuza uchumi wa wanachama na wananchi lakini ndoto zimekatishwa na mgogoro na kukosa eneo la uwekezaji na serikali kukosa mapato.
Hata hivyo Ulomi, alipongeza uongozi wa serikali ya wilaya chini ya Mkuu wa Wilaya Lengai Ole Sabaya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Yohana Sintoo kwa kupambana na ubadhilifu na kutoa haki kwa wanyonge pamoja utatuzi wa migogoro iliyodumu kwa muda mrefu.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai