Wanafunzi 42,000 wa shule za msingi ndani ya wilaya ya Hai wenye umri kuanzia miaka mitano hadi 14 wanatarajia kupewa kingatiba kwa ajili ya kuzuia ugonjwa wa minyoo.
Hayo yamesemwa na mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele katika halmashauri ya wilaya ya Hai Dkt. Apolnary Tesha alipokutana na walimu pamoja na wataalamu wa Afya kwenye ukumbi wa chuo cha Kilimanjaro Modern kwa ajili ya semina ya utoaji wa kingatiba kwa wanafunzi wa shule za msingi.
Dkt. Tesha amesema kuwa zoezi hilo ni muhimu kwa kuwa linakwenda kuzuia magonjwa ambayo yamekuwa yakiathiri watoto kutokana na mazingira ambayo wamekuwa wakiishi ambapo wengi wao hupata magonjwa ya minyoo yanayopelekea upungufu wa damu.
"Tatizo la minyoo ni tatizo kubwa linalozuia wanafunzi kukua kiakili na kimwili ambapo leo tumefanya mafunzo na lengo kubwa la mafunzo haya ni kuwaandaa kwa ajili ya zoezi lililopo mbele yetu ambapo jumatatu Novemba 28, 2022 tunategemea kutoa dawa ya kingatiba ya minyoo katika shule za msingi za Serikali na zile za binafsi kwa wanafunzi wote kuanzia miaka mitano hadi 14" amesema Dkt. Tesha
"Wito wangu kwa wazazi na walezi ni kwamba wawaruhusu watoto wao wafike shuleni siku hiyo ya tarehe 28 Novemba, 2022 kwa ajili ya kupewa kingatiba ya minyoo na wale ambao hawajaandikishwa shule, wapo majumbani hata kama wamemaliza darasa la 7 wazazi wawasisitize waende katika shule zilizopo karibu wakameze dawa za minyoo" ameongeza Dkt. Tesha
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai