Afisa tawala wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Mary Mnyawi amewasihi wanaume kujitokeza kupima afya kwa pamoja na wake zao huku akiwataka kuacha kutegemea majibu ya wake zao pale wanapokwenda kupima afya hasa wakati wa ujauzito.
Mnyawi ameyasema hayo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambayo huadhimishwa duniani kote Disemba 01 ya kila mwaka ambapo katika wilaya ya Hai maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya Snow view Bomang’ombe.
“wanaume msitegemee kwamba majibu ya wake zenu wanapokwenda kupima ndiyo majibu ambayo yanatosha kukuonyesha wewe upo salama, na kama yeye je anao? Lakini inawezekana mmoja akapata na mwingine asipate inategemea na kinga ya mtu ilivyo” amesema Afisa tawala Mnyawi
“kwahiyo ninawasihi sana muwe na tabia ya kwenda kupima kwa pamoja ili kuona na kujua afya zetu zikoje ili baada ya hapo pia tuweze kuelimishwa na kujua namna gani ya kuenenda nab ado tunakuwa na muda mrefu tu wa kuishi hapa duniani vinginevyo ni rahisi kudondoka kwa ghafla kwa kuwa hujafanya kile ambacho ungeelekezwa na wataalamu wa afya”
Akizungumzia mapambano dhidi ya Ukimwi, Mnyawi ameeleza kuwa wilaya hiyo imefanikiwa kuwaanzishia dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo ARV’s asilimia 94% ya waathirika kati ya 95% ya waathirika waliogundulika kuambukizwa.
Siku ya Ukimwi jumla ya watu 736 walipimwa katika wilaya ya Hai, wanaume wakiwa 242 na wanawake 494 ambapo waliogundulika kuwa na maambukizi ni ya VVU ni 15, wanaume 6 na wanawake 9 hali ambayo inaonyesha kushuka kwa maambukizi kwani waliopima ni wengi ila waliogundulika kuambukizwa ni wachache.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, makamo wa mwenyekiti Halmashauri ya wilaya ya Hai Swalehe Kombo Sway ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya kudhibiti Ukimwi wilayani humo anasema kwamba “tumekaa, tumejaribu kupanua wigo mpana wa kuhakikisha kwamba jamii nzima ya wilaya ya Hai inapata elimu ya kutosha juu ya ugonjwa huo”
Mratibu wa ukimwi hospitali ya Hai Dkt. Macha wakati akitoa taarifa ya hali ya ugonjwa huo ameeleza kuwa kuna mwitikio hasi kwa wanaume kwamba majibu ya wenza wao ndiyo majibu yao, hali ambayo imekuwa ikidhoofisha jitihada za Serikali katika kufikia malengo ya kutokuwa na maambukizi mapya ifikapo mwaka 2030.
Mganga mkuu wa wilaya ya Hai Dkt. Itikija Msuya amewataka wale wote ambao tayari wameambukizwa virusi vya ugonjwa huo kufuata kwa usahihi maelekezo na kanuni za kitabibu ili maisha yaendelee kama kawaida kwani wapo watu wengi ambao wameambukizwa lakini wanafuata maelekezo ya wataalamu wa afya na wanaendelea kuishi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai