Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro inaendelea kuimarisha vita ya kupambana na uharibifu wa mazingira ikiwemo kukata miti kwa ajili ya nishati ya kuni au mkaa kwa kutafuta vyanzo mbadala vya nishati.
Akizungumzia mpango huo Afisa Mazingira wa wilaya hiyo Alfred Njegite amesema inawezekana jamii kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa kama chanzo cha nishati kwani vipo vyanzo vingine vya nishati ambavyo vinaweza kusaidia jamii kufanikisha shughuli zao.
Amesema upo uwezekano wa kutumia nishati ya jua, nishati ya mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya nafaka kama pumba na nyingine ambazo zikizoeleka kutumiwa na jamii zitasaidia kupunguza na hatimaye kuondoa uharibufu wa mazingira.
Naye Afisa Maliasili wa wilaya ya Hai Mbayani Mollel amehimiza jamii kuchagua njia mbadala za kupata nishati ili kuendelea kutunza miti na hatimaye kunufaika na faida za uwepo wa miti ikiwemo kupata mvua, kivuli, matunda na nyingine.
Aidha ameipongeza shule ya sekondari Mlangarini ya mkoani Arusha kwa kuanza kutumia teknolojia ya makaa ya mawe kama chanzo cha nishati inayotumika jikoni kwenye maandalizi ya chakula cha walimu na wanafunzi.
Akizungumza kwenye ziara ya kuona mafanikio ya kutumia makaa ya mawe Mkurugenzi wa kampuni ya Ashael Investment inayojishughulisha na kutengeneza na kusambaza teknolojia ya makaa ya mawe Ashael Lukumay amesema kuwa matumizi ya makaa hayo yanasaidia kutunza mazingira kwa kuepusha kukata miti ya kuni na mkaa ikiwa ni pamoja na kutunza usafi wa mahali yanapotumika.
Shule ya sekondari Mlangarini ni moja ya taasisi zinazotumia teknolojia ya makaa ya mawe kutoka kampuni ya Ashael investment na kufaidika pamoja na faida nyingine ni kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumika kwenye mnyororo wa kuni kuanzia kununua, kusafirisha pamoja na kukata vipimo vya kutosha jikoni.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai