Watumishi wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia taratibu za kazi na kuboresha huduma wanazowapatia wananchi ikiwa ni sehemu yao katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inaoongozwa na Dr John Pombe Magufuli.
Wito huo umetolewa kwenye ziara ya kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Hai iliyokagua utekelezaji wa shughuli za serikali katika wilaya ya Hai kupitia miradi ya maendeleo inayofanywa na halmashauri.
Akizungumza kwenye ziara hiyo; Katibu wa CCM Wilaya ya Hai Kumotola Kumotola amesema ni jukumu la kila mtumishi wa umma kuongeza ufanisi kwenye eneo lake la kazi ili kuendana na kasi ya serikali katika kuwahudumia wananchi wake.
Kumotola ameipongeza Idara ya Afya kwa kufanikiwa kutekeleza miradi yake kwa kiwango cha kuridhisha ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kwa duka la dawa ndani ya hospitali ya wilaya na kukamilika kwa wodi za wanawake.
Kumotola pia amemtaka Mganga Mkuu wa Wilaya kuendelea kudhibiti suala la lugha isiyoridhisha lililokuwa likilalamikiwa na wagonjwa wanaopatiwa huduma katika hospitali hiyo.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Irine Haule ametoa shukrani kwa Rais Magufuli kwa kutoa vitanda vya kujifungulia kwa wodi za wajawazito pamoja vitanda vya kulalia wagonjwa wa kawaida huku akiishukuru kamati hiyo kwa kutoa changamoto katika hospitali ambazo zimekuwa zikifanyiwa kazi siku hadi siku na kuisaidia kusonga mbele.
Pamoja na pongezi hizo; kamati hiyo ya siasa imebaini changamoto mbalimbali kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo hali ya uchafu wa mazingira yanayozunguka maabara, utunzaji hafifu wa mali na vifaa pamoja na usimamizi usioridhisha kwa mafundi kwenye mirad ya ujenzi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edward Ntakilio amesema kuwa amezipokea changamoto zilizotolewa na kamati hiyo na kuahidi kuzifanyia kazi ili kuboresha ufanisi katika utendaji wa kazi na kuwakumbusha watendaji wa serikali kuwa wanao wajibu wa kuwatumikia wananchi kwa upendo.
Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Hai imefanya ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kwenye wilaya hiyo kwa lengo la kufahamu ni kwa kiasi gani halmashauri inatekeleza miradi kulingana na ilani ya uchaguzi ya chama hicho ambapo ilitembelea ujenzi wa maabara ya shule za sekondari Rundugai na Longoi, ujenzi wa Kituo cha afya Chekimaji, Kikundi cha uhifadhi mazingira cha Iroko, kikundi cha wakina mama wafugaji ebeneza kilichopo Nronga, jengo la kusindika Vanila, pamoja na hospitali ya wilaya ya Hai.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai