"Lazima tuhakikishe tunaongeza bidii katika ukusanyaji wetu wa mapato ikiwa ni pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato katika halmashauri yetu ya wilaya ya Hai, bado sijaridhishwa na ukusanyaji huu" Dc Hai - Juma Irando.
Mkuu wa Wilaya ya Hai Juma Irando amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuimarisha makusanyo yake ili kuendelea kuihudumia jamii.
Irando ameyasema hayo mapema hii leo wakati akizungumza na watumishi wa makao makuu ya halmashauri ya Hai ambapo mbali na kuwataka kufanya kazi kwa bidii pia ameelezea kutokuridhishwa na hali ya ukusanyaji wa mapato huku akitaka jitihada zaidi za kuimarisha ukusanyaji zichukuliwe.
Aidha amewataka watumishi kufanya kazi kwa uhuru na kushirikiana huku akisema kuwa atakuwa mstari wa mbele katika kutoa ushirikiano ili kuleta ufanisi zaidi.
Mkuu huyo wa wilaya pia amewataka wataalamu wa idara ya ardhi kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu ili kuondoa kero kwa wananchi ikiwemo kugawa eneo moja mara mbili kwa watu tofauti jambo linalosababisha migogoro ya ardhi.
Awali akimkaribisha mkuu huyo wa wilaya, Katibu tawala wilaya ya Hai Upendo Wella amewataka watumishi na taasisi za umma kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuimarisha huduma zitolewazo kwa jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amemhakikishia Mkuu wa Wilaya ushirikiano wa wakuu wa idara na watumishi wote wa halmashauri akibainisha kuwa watumishi wapo tayari kutimiza wajibu wao na kuweka mchango wao katika kuboresha huduma zinazotolewa kwa jamii.
Kikao hiki ni cha kwanza ambacho Mkuu wa Wilaya amekitumia kujitambulisha lakini pia kuweka mikakati ya pamoja na watumishi kuhusu namna ya kutekeleza majukumu yaliyo mbele yao ya kuwahudumia wananchi wa Wilaya ya Hai.