Wito umetolewa kwa watanzania kumuenzi kwa vitendo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa kufanya mambo ambayo aliyasimamia na kuyaamini kuwa yataleta maendeleo kwa Taifa.
Akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Hai kwenye maadhimisho ya Siku ya Vijana na Kumbukizi ya Baba wa Taifa; Afisa Tarafa wa Masama Nsajigwa Ndagile amesema ni wajibu wa wananchi wote kila mmoja kwa eneo lake kufanya kazi ili kufanikisha maono ya Mwalimu Nyerere kwa Taifa la Tanzania.
Nsajigwa amesema kuwa Nyerere aliamini kwamba kufanya kazi kwa bidi kutaondoa utegemezi wa mtu mmoja mmoja na hatimaye kwa nchi nzima na kwamba kazi ndiyo msingi wa maendeleo.
Ameongeza kuwa Baba wa Taifa alianzisha mapambano dhidi ya maadui ujinga, maradhi na umasikini pamoja na rushwa aliyoitambulisha kama adui wa haki na maendeleo; na kuwataka wananchi kuendeleza mapambano hayo kwa manufaa ya nchi yao.
“Leo hatumkumbuki Mwalimu Nyerere kwa sababu ya idadi ya nyumba au magari aliyomiliki bali kwa sababu ya mchango wake katika maendeleo ya nchi hii” ameongeza Nsajigwa.
Aidha Nsajigwa ametumia jukwaa hilo kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa namna inavyochangia kuinua vijana kiuchumi kwa kuwapatia mikopo, kuwakutanisha na elimu ya ujasiriamali na namna ya kupata masoko ya bidhaa zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo, amesema halmashauri yake itaendelea kutoa mikopo kwa vijana na makundi mengine ya wanawake na watu wenye ulemavu ili kuwainua kiuchumi.
Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani; Sintoo amewataka wananchi kujitokeza kusikiliza sera za wagombea ili kujiongezea uelewa wa kufanya maamuzi sahihi ya kuchagua kiongozi anayefaa siku ya kupiga kura.
Sintoo ametumia maadhimisho hayo kucheza moja ya hotuba za Mwalimu Nyerere inayowakumbusha wananchi kuwaepuka wagombea wanaowashawishi kuwachagua kwa misingi ya ukabila na Imani za kidini.
Halmashauri ya Wilaya ya Hai imefanya maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Vijana na Kumbukizi ya Kifo cha Baba wa Taifa kwa kufanya mdahalo wa wanafunzi, maonesho ya kazi za vijana katika ubunifu, Sanaa, biashara na ujasiriamali pamoja na hotuba za viongozi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai