Bilionea Saniniu Laizer hii leo amekabidhi kiasi cha shilingi milioni kumi (10,000,000) alizoahidi kwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya walipokutana hivi karibuni kama mchango wake wa kuendeleza ujenzi wa ukumbi wa kisasa wa Jeshi la polisi katika kituo cha polisi Bomang’ombe.
Akikabidhi fedha hizo kwa niaba ya Bilionea Laizer aliyekuwa diwani wa kata ya Naisinyai wilayani Simanjiro Clamp Laizer amesema kuwa bilionea lazier ametoa fedha hizo akitambua mchango wa jeshi la polisi hasa katika ulinzi wa raia na mali zao huku pia akisema ameunga mkono juhudi zilizoanzishwa na mkuu wa wilaya hiyo.
Akipokea fedha hizo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Afisa Tawala Marry Muyawi amemshukuru bilionea Lazier kwa kukamilisha ahadi yake na kusema kuwa fedha hizo zitasaidia kuendeleza ujenzi wa jengo hilo ambalo kukamilika kwake kutasaidia matumizi mbalimbali kama vile mikutano ya jeshi hilo.
Naye Mkuu wa polisi Bomang’ombe afande Lwelwe Mpina amesema kuwa fedha hizo zitaimarisha ujenzi wa ukumbi huo ambapo pia amemshukuru Mkuu wa wilaya ya Hai aliyeanzisha mchakato wa ujenzi huo ambao hadi hapa lilipofikia hatua ya kuwekezwa bati.
Aidha Mpina amebainisha kuwa tayari ameshajitokeza mfadhili wa atakayechangia bati za kuezekea jengo hilo hivyo fedha zilizotolewa na bilionea Laizer zitatumika kukamilisha kipande kingine kilichosalia.
Ikumbukwe kuwa ujenzi wa ukumbi huo ulianzishwa mwezi wa sita mwaka jana kwa jitihada za mkuu wa wilaya ya Hai baada ya kuelezwa kuwa jeshi la polisi wilayani hapa linakabiliwa na changamoto hiyo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai