Mkuu wa wilaya ya Hai Mhe. Amiri Mkalipa amewataka madereva bodaboda na bajaj wilayani humo kutojaribu kujihusisha na makundi ya kihalifu kwa namna yoyote ile na atakayebainika kujihusisha atachukuliwa hatua za kisheria.
Mkalipa ametoa rai hiyo alipozungumza na madereva hao Februari 23, 2023 kwenye ukumbi wa polisi Bomang'ombe wilayani Hai na kuwataka kuithamini tasnia ya udereva ikiwa ni pamoja kutokutumia vyombo vyao kwenye mambo uhalifu.
"Mimi ni sehemu ya nyinyi na nyinyi ni sehemu ya Mimi, kitu nisichotaka ni madereva wa boda boda wa Hai na madereva wa bajaj wa Hai kujihusisha na makundi ya wahalifu, usitumie chombo chako kwenye jambo la uhalifu tutakuchukulia hatua za kisheria"
"Kama ilivyo kauli mbiu ya Kazi iendelee, twendeni tukapige kazi, anayefanikiwa duniani ni yule anayefanya kazi na akaamini kazi yake inaweza kumtoa hatua moja kwenda nyingine, hakuna aliyeanzia juu, hata mbuyu ulianza kama mchicha"
Naye mkuu wa Polisi wilaya ya Hai Mrakibu mwandamizi wa Polisi SSP Juma Majatta amewataka kujihakikishia usalama wao kwanza kwa kutosafirisha abiria katika maeneo ambayo ni hatarishi hususani nyakati za usiku.
"Wengine mnaowabeba siyo watu wazuri, kuna baadhi ya madereva bodaboda na bajaj wanafanya kazi masaa 24, kumi na moja alfajiri yuko barabarani hajui anambeba nani na anamsafirisha nani kitu ambacho ni cha hatari sana"
Nao madereva bodaboda na bajaj wilayani humo wamempongeza Mhe. Amiri Mkalipa kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mkuu wa wilaya ya Hai na kuahidi kumpa ushirikiano katika majukumu yake ya kazi wilayani humo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai