SERIKALI wilayani Hai, Mkoani Kilimanjaro imewataka viongozi wa Halmashauri hiyo kusimamia agizo la Rais John Magufuli la kutowatoza ushuru wa mazao kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo kwani jambo hilo limekuwa likiwakandamiza watanzania wanyonge.
Mkuu wa wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wafanyabiashara katika soko la matunda na mbogamboga la Kwa sadala ambapo aliwataka watumishi hao kuhakikisha kuwa wanaheshimu agizo la Rais alilolitoa Aprili 29 mwaka 2016 na kusisitiza kuwa agizo hilo ni lazima liheshimiwe na endapo kutabainika mtumishi yoyote kuendelea kuwatoza ushuru wakulima hao wadogo hatua kali zitachukuliwa.
" Lazima viongozi wote kuheshimu agizo la Rais wetu ambae ameamua kuwakomboa wakulima kwa kufuta ushuru hivyo tambueni kuwa kauli ya Rais ni Agizo" alisema Ole Sabaya.
Akizungumzia suala la usafi katika soko hilo, Sabaya aliitaka Idara ya Usafi na Mazingira ya Wilaya hiyo kuhakikisha kuwa wanazoa taka zote zilizoko katika soko hilo kabla ya Oktoba 9 mwaka huu ili kuepusha magonjwa ya mlipuko yanayoweza kusababishwa na uchafu.
"Mnachukua ushuru kwa watu hao lakini mnashindwa kuliweka soko katika hali ya usafi naagiza ifikapo siku ya Jumanne uchafu wote uwe umetolewa na mkishindwa msitoze ushuru kwa wafanyabiashara hawa"alisisitiza Ole Sabaya.
Mkuu wa Wilaya anaendelea na ziara za kikazi za kutembelea maeneo mbalimbali ambapo katika soko la Kwa Sadala amepata fursa ya kuzungumza na wananchi wakiwemo wafanya biashara kwenye soko hilo ili kufahamu changamoto wanazokutana nazo lakini pia kuwahimiza kuendelea kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu” inayosimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayowataka watu wote wafanye kazi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai