Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya ameagiza kukamatwa na kuchunguzwa kwa baadhi ya waliokuwa wajumbe wa halmashauri ya Kijiji cha Mijongweni, baadhi ya viongozi wa bodi ya ushirika, baadhi ya wajumbe wa kamati ya mpito iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya na kukusanya fedha za ushirika pamoja na waliouza na kununua pawa tila ‘power tiller’ ya kijiji hicho katika Kata ya Mnadani kwa tuhuma za ubadhirifu wa shilingi milioni 274.
Sabaya ametoa agizo hilo akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kwenye mkutano wa kupokea ripoti ya tume ya uchunguzi iliyoundwa kufuatilia ubadhirifu wa vifaa vya kilimo na matumizi mabaya ya fedha za wanakijiji.
Waliokamatwa ni pamoja Abuu Fujo, Salama Mwingira, Deogratias Kimaro na Sadick Msangi ambao walikuwa ni wajumbe wa kamati ya fedha na wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji, wajumbe wa bodi ya ushirika ambao ni Nuru Juma, Mayunga Mathayo, Richard Msele na Adam Mdaki.
Wengine ni Alex Mkwizu na Miraji Araba ambao ni wajumbe wa kamati iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kukusanya makusanyo yanayotokana na umwagiliaji na kundi la mwisho ni mnunuzi wa power tiller ya kijiji Kuswai Mrisha na Bakari Mloka anayetuhumiwa kuuza power tiller hiyo.
Awali akisoma ripoti ya tume ya uchunguzi iliyoundwa kufuatilia huo; Mwenyekiti wa kamati hiyo Valeria Banda amebainisha majibu yaliyopatikana wakati wa uchunguzi huo.
Amesema kamati hiyo ilibaini kuwa Power Tiler aina ya KUBOTA yenye thamani ya milioni 17 iliyotolewa na Wizara ya Kilimo kwa halamashuri ya wilaya ya Hai kwa kikundi cha mkombozi iliuzwa kinyemela kwa Yusufu Ndesindilo mkazi wa Moshi Mjini na fedha iliyopatikana haijulikani ilipopelekwa huku vipuri vya mashine zilizoletwa vikiibiwa na kusababisha hasara.
Banda ameongeza kwamba kamati yake ilibaini kuwa usimamizi wa mashine za kuvuna mpunga shambani haukuwa mzuri kutokana na baadhi ya wajumbe wa bodi kujipangia zamu kimaslahi huku wengine wakivuna nyakati za usiku na kutopeleka hesabu za fedha.
Aidha amebainisha kuwa kamati ilibaini kuwa fedha zilizokuwa zikipatikana shambani zilikuwa zikifanya kazi zisizojulikana huku kiasi kingine kikipelekwa saccos ya Jitegemee na kutolewa kwa wakati huohuo na kuingizwa katika matumizi mengine yasiyokuwa na kibali bila kufikishwa ofisini.
Mara baada ya uwasilishwaji wa taarifa hiyo Mkuu wa Wilaya hiyo Lengai Ole Sabaya amewataka wananchi wa kijiji hicho kutambua kuwa utaratibu uliokuwa unafuatwa wa kuwasajili watu kwa kulipa hela kuwa ni batili kwani serikali ilitoa mashine hizo bila ya mahariti hayo.
Katika hatua hiyo Mkuu huyo wa wilaya aliagiza jeshi la polisi kumkamata Afisa ushirika Mstaafu wilaya Rafaeli Mmbwambo ili kujibu baadhi ya tuhuma zinazomkabili kutokana na yeye kuwa mlezi wa chama hicho huku akipewa kiasi cha shilingi laki mbili kufanya marekebisho ya masharti lakini hadi sasa chama hicho hakina masharti.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai