Mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya amewataka watumishi wa Umma wilayani hapo kuongeza juhudi na maarifa katika kuwatumikia wananchi hususani kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii.
Sabaya ametoa wito huo katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo kwa lengo la kumkaribisha ofisini baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kushika wadhifa huo.
Amesema watumishi wa umma wanatakiwa kukumbuka kuwa wameajiriwa na mwananchi ambaye anatumia nguvu zake kulipa kodi hivyo ni lazima watumishi kuweka mbele maslahi mapana ya wananchi wanaowahudumia badala ya kuangalia maslahi yao binafsi.
Amesema yupo tayari kushirikiana na kila kundi linalohusika kuhakikisha kuwa mwananchi wa Wilaya ya Hai anapata huduma anazostahili ikiwemo elimu, afya, maji, miundombinu na huduma nyingine.
“Nitashirikiana na Katibu wa CCM na Kamati ya Siasa, nitashirikiana na vyama vyote vya siasa vilivyopo, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkurugenzi na watumishi walio chini yake; tukutane tujadiliane namna ya kutatua kero za wananchi badala ya kupoteza nguvu kugombana” ameongeza Sabaya.
Aidha Sabaya ametoa wito kwa wanasiasa hususani madiwani kutumia nafasi walizonazo kusaidia kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha kwa kutatua kero mbalimbali walizonazo.
“Kipimo kikubwa kwa wananchi ili uendelee kuwa kiongozi wao sio mavazi, uwezo wa kuongea wala nguvu unazotumia kuwashambulia watumishi wa halmashauri bali wanaangalia namna unavyowasaidia kutatua changamoto zinazowakabili” ameongeza.
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Hai Kumotola Kumotola amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa kuonesha nia ya kushughulika na matatizo ya wananchi kwani Chama Cha Mapinduzi kinachoongoza Serikali ni chama chenye kuwajali wananchi wake.
Amemwomba Mkuu wa Wilaya kutatua kero zinazowasumbua wananchi kwa muda mrefu katika migogoro ya ardhi pamoja na uhaba wa maji hasa kwenye ukanda wa tambarare wa wilaya.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya hafla hiyo Diwani wa Kata ya Bomang’ombe Joel Nkya amesema Mkuu wa Wilaya ametoa hotuba yenye muelekeo inayoamsha matumaini ya wananchi kwa namna anavyojipanga kuwatumikia wananchi kwa kutatua kero zao.
Amesema anayo imani watashirikiana vizuri katika kuwahudumia wananchi wa Wilaya hiyo huku akibainisha kuwa wamepokea wito wa Mkuu wa Wilaya wa kushauriana namna ya kuboresha huduma kwa wananchi.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amebainisha furaha yake kupata kiongozi wa wilaya na kwamba ofisi yake na watumishi walio chini yake watampa ushirikiano na watamuunga mkono katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika kuwahudumia wananchi na kuwaletea maendeleo.
Sintoo amesema amepokea maagizo yaliyotolewa na kiongozi wa wilaya na kwamba yeye na wataalamu walio kwenye ofisi yake wao wajibu wa kutekeleza maagizo hayo kwa manufaa ya wananchi wanaowahudumia.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai