Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Onesmo Buswelu amewataka wazazi wilayani humo kuitikia mwito wa kuwapeleka watoto wao kupatiwa chanjo ili kuwakinga na magonjwa mbalimbali wanapofikisha umri wa kupatiwa chanjo hizo.
Ametoa rai hiyo wakati wa kuzindua utoaji wa chanjo ya sindano ya ugonjwa wa Polio kwa watoto wenye umri wa wiki 14 pamoja na chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi inayotolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 9 uliofanyika kwenye hospitali ya Wilaya ya Hai leo 27/04/2018.
Akizungumza na wananchi waliofika hospitalini hapo na watoto wao kupata chanjo ya ugonjwa wa Polio kwa sindano, Buswelu amesema wapuuze upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu wanaotaka kuwapotosha na kuwasababishia kuwakosesha watoto wao haki ya kuishi bila magojwa kwani chanjo hii inamkinga mtoto na magonjwa ya kupooza.
Aidha Buswelu amezungumzia chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi wanayopatiwa wasichana wa umri wa miaka 9 akisema kuwa siyo kitu kipya mkoani Kilimanjaro kwani ilianza kutolewa tangu mwaka 2014 na ilitolewa kwa wasichana wa miaka 9 hadi 14 tofauti na mikoa mingine ambayo chanjo hiyo inaanza mwaka huu.
Biswelu pia amewakumbusha watumishi wanaotoa huduma za afya kutimiza jukumu lao kuu la kuwapatia chanjo walengwa na wasisimamie kwenye kufikisha lengo la takwimu pekee lakini pia kuzitunza kwani zimepatikana kwa fedha nyingi.
“Chanjo hii hatulipii chochote sisi wenye watoto; lakini serikali inagharamia fedha nyingi kwa ajili ya watoto hawa. Kodi zetu zinazokusanywa na serikali ndizo zinazotumika kupata chanjo hii. Serikali ipo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wake”. Amesisitiza Buswelu.
Akitoa utangulizi kuhusu chanjo hizo; Mratibu wa Chanjo Wilaya ya Hai Michael Ndowa amesema kuwa chanjo ni njia madhubuti ya kudhibiti magonjwa kwani kuipata kabla ya maambukizi kunamuepusha mhusika kupata maambukizi ya ugonjwa lakini pia haina gharama kwa mwananchi kwani inagharamiwa na serikali kwa asilimia mia.
Ndowa amesema kuwa jumla ya vituo 62 vya huduma za afya na shule za msingi 128 katika wilaya vitatumiwa katika kufanikisha kazi ya kutoa huduma za chanjo hizo ambapo kwa wasichana wanaopatiwa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi watafikiwa shuleni na kupatiwa huduma hiyo.
Kwa upande wake kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai Dkt. Irene Haule amewakubusha viongozi wa dini na viongozi wa kijamii kutimiza wajibu wake kwa kuhamasisha na kuhakikisha kila mtoto anayefikisha miezi 14 anapelekwa kupata chanjo hiyo lakini pia wasichana wa miaka 9 waliopo shuleni na wale ambao hawasomi.