DC Sabaya Aingilia Kati Mwili wa Marehemu Ulioshikiliwa KCMC
Imetumwa: May 8th, 2021
Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya leo Mei 8, 2021 amemuagiza Katibu Tawala wa wilaya hiyo Upendo Wella kusimamia zoezi la kuchukua mwili wa Bauda Nkya (68) mkazi wa Kijiji cha Nshara kata ya Machame Kaskazini ambaye mwili wake umezuiliwa chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya KCMC kwa kukosa fedha za matibabu.
Sabaya ametoa maagizo hayo alipofika nyumbani kwa marehemu Bauda Nkya kwa lengo la kusikiliza malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha Nshara waloonesha kuhuzunishwa na kitendo cha mwili wa mpendwa wao kuzuiliwa.
Waombolezaji hao wamedai kuwa mwili wa mpendwa wao ulizuiliwa katika hospitali ya KCMC baada ya familia yake kushindwa kulipa malipo ya huduma za matibabu waliyokuwa wakidaiwa na hospitali hiyo na kuamua kuchangisha fedha na kufikisha shilingi milioni moja na laki mbili (1,200,000).
"Poleni kwa msiba na hongereni kwa kuweza kuchangia kiasi cha shilingi milioni moja na laki mbili; huu ni mfano mzuri wa ushirikiano. Kiasi kilichobaki ofisi yangu itagharamia ikiwa ni pamoja na kufanikisha mwili kuruhusiwa huko uliposhikiliwa.” Amesema Sabaya.
“Mambo mengine ni ya kibinadamu tu, Bibi huyu (marehemu) alikuwa ni mnufaika wa TASAF na hali ya hapa kwake inaonekana, kupata shilingi milioni 3 ni shida nyingine kwa familia hii, hivyo Mwenyekiti wa Kijiji utashirikiana na DAS (Katibu Tawala Wilaya) kutoka ofisi yangu kufanya taratibu zote na kesho Mei 9.2021 mwili upumzishwe" Ameongeza DC Sabaya.
Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu Muzaimata Urassa ameeleza kuwa mama yao alikuwa akisumbuliwa na mguu baada ya kujikwaa kwenye kisiki na kupelekea mguu wake kuoza ambapo alifariki Mei 2 mwaka huu na mwili kuchukua wiki moja bila kuzikwa kutokana na changamoto ya familia kukosa fedha.
Tukio hilo limeleta simanzi zaidi kwa familia na waombolezaji ambao wamesema kuwa mwili wa marehemu ulipaswa kusitiriwa mapema ikiwa pia ni kwa mujibu wa imani yao ya dini ya Kiislamu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya KCMC Dkt Gilead Masenga alipopigiwa simu kuzungumzia tukio la kuzuiliwa kwa mwili huo; amesema kuwa hawajawahi kupokea maombi kutoka kwa familia hiyo na kubainisha kuwa kama familia inashindwa kulipia gharama kama hizo wanapaswa kufuata taratibu zilizopo jambo ambalo halikufanyika.
Taratibu zinazofahamika ni kwa ndugu wa marehemu kuwasilisha maombi ya kupatiwa msamaha wa malipo kupitia afisa ustawi wa jamii wa hospitali hiyo ambaye atajiridhisha maombi ya familia na kuruhusu mwili kuchukuliwa.
Mkuu wa Wilaya ametoa maelekezo kwa hospitali kutumia busara kushughulikia masuala ya ndugu wa marehemu kukosa fedha badala ya kuzuia mwili kwani kufanya hivyo kunaongeza machungu kwa wafiwa.