Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya ameruhusu kuendelea kwa shughuli za uchimbaji wa madini ya mchanga baada ya kusitisha kwa siku kadhaa kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira hali iloyopelekea kuhatarisha maisha ya wananchi waliokuwa katika maeneo hayo.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliyofanyika katika mji mdogo wa Bomang’ombe, Sabaya amesema kuwa migodi ambayo imeruhusiwa kuendelea na uchimbaji ni ile ambayo haina uhatarishi wowote kwa wachimbaji na jamii kwa ujumla.
“Nikiona kitu chochote kinachoweza kusababisha hatari katika maisha ya wananchi nina wajibu wa kuzuia isitokee, ndio maana nilizuia machimbo haya kwa muda. Mazingira ya mashimo mnayochimba si ya kuridhisha na yanahatarisha usalama wa wananchi.” Amesema Sabaya.
“Baada ya kushauriana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya; tumekubaliana kufungulia migodi ambayo haina hatari kwenye usalama wa wananchi, kwa ile migodi yenye hatari nimetoa kibali cha siku thelathini ili ifukiwe. Wakati mnachimba migodi mingine muhakikishe mnafukia zile ngema zote kwa sababu zile ni hatari sana.” Amebainisha Dc Sabaya.
Aidha amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai pamoja na Afisa Mazingira wilaya kufika katika eneo la uchimbaji kwa ajili ya kuwaonyesha wachimbaji maeneo sahihi ya uchimbaji wa madini hayo.
Katika kushughulikia kero mbalimbali za wananchi kwenye sekta ya ardhi, Mkuu wa Wilaya Sabaya amewaahidi wananchi kuwa atatafuta siku maalumu ya kushughulikia kero hizo.
“Kuhusu migogoro ya ardhi naagiza Afisa Ardhi kupitia ofisi ya Mkurugenzi, mshirikishe wenyeviti wote na wanachi watangaziwe tupate malalamiko yote ya ardhi tuyafanyie kazi, tutenge siku mbili (ardhi day) za kutatua kero zote za ardhi Wilaya ya Hai ambapo tutasikiliza malalamiko yote ya ardhi na kufanya maamuzi. Kwa kesi zitakazotakiwa kwenda mahakamani tutashauri hivyo ili tuweze kumaliza malalamiko yote.”
Hivi karibuni Kamati ya ulinzi na usalama wilayani Hai ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ilifika katika maeneo ya uchimbaji wa madini hayo kuona namna shughuli zinavyoendeshwa na kugundua kuwa eneo hilo linahatarisha usalama wa wachimbaji na wananchi wanaozunguka maeneo hayo na kuagiza shughuli hizo kusitishwa kwa muda.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai