MKUU wa wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya amewataka wanafunzi wa shule za sekondari wilayani humo kuzingatia masomo na kuacha kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi hali ambayo imekuwa ikisababisha kukatisha masomo kwa kupata mimba na kusababisha hasara kwa familia na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Wasichana ya Machame wakati wa uzinduzi wa wiki ya upandaji miti Ole Sabaya amesema kuwa tatizo la mimba kwa wanafunzi limechangiwa sana na wanafunzi kujiingiza katika mahusiano kwenye umri mdogo na kusahau jukumu lao la msingi la kusoma.
Amesema kuwa wanafunzi kupata mimba wakati wa masomo ni kulitia doa Taifa pamoja shule kwani lazima kila mmoja ahakikishe anasoma kwa malengo ili kuondokana ili kuepuka tatizo hilo.
Hata hivyo amelitaka jeshi la polisi kuhakikisha kuwa linamkamata mtu anayetuhumiwa kumsababishia ujauzito mwanafunzi ili afikishwe mahakamani kujibu mashitaka ya kosa la ubakaji.
“Huyu ni mbakaji kama wabakaji wengine; kwa hiyo akamatwe na afunguliwe mashitaka hayo ili sharia ichukue nafasi yake” Ameagiza Ole Sabaya.
Amewataka wanafunzi kuhakikisha kuwa wanajitunza na kusoma kwa bidii ili kutumiza ndoto zao na kuweza kuwa wataalumu wa baadae.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Hai Upendo Wella amewataka wanafunzi wote hasa wasichana kusoma kwa bidii ili kuweza kulitumikia Taifa katika nyanja mbalimbali wakati muafaka ukifika.
Akizungumzia zoezi la upandaji miti Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amesema kuwa halmashauri yake inao utamaduni wa kupanda miti kila tarehe 01 mwezi 04 ya kila mwaka kwa kuzingatia maelekezo ya serikali na kwa mwaka huu imepangwa kupanda miti zaidi milioni moja na nusu katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya taasisi za umma na binafsi.
Sintoo amesema kuwa miti inayopandwa katika msimu huu itahakikishiwa kutunzwa na kukua kwa ajili ya kuboresha mazingira pamoja kukabiliana na ukame unaoweza kujitokeza kutokana na ukosefu wa miti.
Naye Mkuu wa Shule ya Wasichana Machame Mwalimu Asteria Massawe ameshukuru kwa serikali kuadhimisha siku ya upandaji miti shuleni kwake na kuahidi kusimamia kwa uaminifu utunzaji wa miti iliyopandwa.
Awali, akisoma taarifa kwa mgeni rasmi, Afisa Misitu Wilaya ya Hai Mbayani Mollel amesema kitendo cha kupanda miti kina manufaa kwa jamii kwa kuinusuru na majanga ya kimazingira lakini pia inasaidia kuimarisha uwiano wa kiasili na kiikolojia baina ya mifumo inayowezesha uhai.
Mollel ameongeza kuwa jumla ya miti 3,000 imepanda siku ya uzinduzi wa wiki ya upandaji miti na kwamba wiki hiyo itatumika kuhamasisha na kufuatilia wananchi kupanda miti kwenye maeneo ya makazi, biashara, mashamba na maeneo ya taasisi pamoja na sehemu zote zenye vyanzo na mkondo wa maji.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai