DCC Yaishauri Halmashauri ya Hai Kuimarisha Vyanzo vya Mapato
Imetumwa: February 16th, 2021
Kamati ya ushauri ya Wilaya (DCC) ya Hai mkoani Kilimanjaro imeishauri wilaya hiyo kubuni vyanzo vipya vya mapato pamoja na kuimarisha vyanzo vya mapato vilivyopo ili kujiongezea uwezo wa kuwahudumia wananchi.
Akizungumza kwenye kikao hicho kilichokuwa na ajenda ya kujadili bajeti ya halmashauri; Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Hai Lawrence Kumotola amesema ili halmashauri iweze kuwahudumia vizuri wananchi kwenye sekta za afya hasa matibabu bure kwa wazee, elimu na sekta nyingine ni lazima kuwe na vyanzo vya uhakika vya kukusanya fedha zitakazofanya huduma hizo.
Ameikumbusha Halmashauri kutekeleza agizo la Serikali la kujenga vituo vya afya kupitia fedha za mapato ya ndani ikiwa ni mkakati wa Serikali kuimarisha utoaji huduma za afya karibu na wananchi huku akibainisha kuwa utekelezaji wa agizo hilo uzingatie maeneo yenye uhitaji zaidi.
Kumotola ametumia kikao hicho kuelezea umuhimu wa kituo cha Redio Boma Hai inayomilikiwa na halmashauri hiyo kuwa inaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato iwapo itafanyiwa maboresho yanayohitajika ikiwa ni pamoja na kuiongezea masafa ili isikike kwenye eneo kubwa na watu wengi zaidi.
Kuhusu uanzishwaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Bomang’ombe; Kumotola ameshauri kufanyike juhudi za makusudi za kupata mamlaka kamili ya mji mdogo huo.
Kikao hicho pia kimeipongeza halmashuri ka namna inavyoendelea kutekeleza majukumu yake ya kuhudumia wananchi, maboresho kwenye sekta ya afya baada ya uzinduzi wa kitengo cha kinywa na meno, Kushika nafasi ya nne kitaifa kwenye matokeo ya mtihani ya Darasa la Saba mwaka 2020, Mamlaka ya Mapato (TRA) Wilaya ya Hai kwa kufanya vizuri kwenye makusanyo ya mapato.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amekiambia kikao hicho kuwa halmashauri yake inapokea ushauri uliotolewa na wajumbe na kwamba wataufanyia kazi ipasavyo kulingana na mazingira ili kuimarisha ufanisi na utoaji huduma kwa wananchi.
Sintoo amesema kuwa halmashauri inasubiri maelekezo ya Serikali kuhusu vyanzo vya mapato vilivyorudishwa kukusanywa na halmashauri ili kuona namna ya kutumia fedha hizo kuboresha huduma za halmashauri ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya na huduma nyingine.
Awali akiwasilisha makisio ya bajeti Afisa Mpango wa halmashauri hiyo Herick Marisham amesema makisio ya bajeti ya halmashauri ya Shilingi 34,766,644,328.00 zitakazopatikana kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo mapato ya ndani, ruzuku ya mishahara, miradi ya maendeleo na vyanzo vingine pamoja na maombi maalumu ya shilingi 1,345,000,000.00 kwa ajili ya kuhudumia shughuli za halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya kimekaa chini ya kaimu Mwenyekiti Upendo Wella ambaye ni Katibu Tawala Wilaya akimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo na wamejadili masuala yanayohusu bajeti ya halmashauri hiyo pamoja na bajeti ya TARURA na kushauri namna ya kuimarisha makusanyo pamoja na kuboresha huduma kwa wananchi.