Diwani Rutaraka Achangia Saruji Ujenzi wa Madarasa
Imetumwa: January 5th, 2021
Diwani wa kata ya Muungano na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka amekabidhi mifuko 20 ya saruji katika shule ya msingi Mlima Shabaha ikiwa ni mchango wake kwa ajili ya ujenzi wa vyumba madarasa.
Rutaraka amekabidhi msaada huo ikiwa ni utekelezaji wa baadhi ya ahadi zake na ahadi iliyopo kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa shuleni hapo.
Rutaraka amebainisha kuwa ni wajibu wake kama kiongozi kuonyesha mfano katika kupeleka maendeleo kwenye kata hiyo ambapo zoezi hilo ni endelevu kwa sehemu nyingine ikiwemo shule ya msingi Kambi ya raha ambapo ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa unaendelea.
“Serikali yetu imeweka utaratibu wa kumalizia ujenzi wa majengo yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi hadi kufikia lenta kisha serikali inaleta fedha za kufanya umaliziaji ikiwemo kupaua” Amesema.
“Sisi kama jamii tunatakiwa kuchangia sehemu yetu ya ujenzi ili fedha za serikali kiasi cha shilingi milioni kumi na saba zinapokuja zifanye kazi ya kupaua na kuweka samani kwa ajili ya watoto wetu kupata sehemu nzuri ya kusomea” Ameongeza Rutaraka.
Akipokea msaada huo Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Coletha Gomezulu amemshukuru diwani huyo kwa mchango wake huku akitoa rai kwa wadau wengine kuendelea kutoa misaada ya hali na mali ili kusaidia ujenzi wa miundombinu ya shule kukamilika kwa wakati hali itakayosaidia wanafunzi kupata mazingira mazuri ya kusomea.
Gomezulu amesema kuwa mpaka sasa jumla ya wanafunzi 24 wa awali wameandikishwa shuleni hapo kati yao wavulana wakiwa ni 12 na wasichana 12 huku wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa idadi yao ni 38 kati yao wavulana ni 22 na wasichana 18 hivyo ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa utasaidia wanafunzi kupata mazingira stahiki ya kupata elimu kikamilifu.
Naye mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Godson Abraham ameeleza kuwa mpaka sasa shule hiyo ina vyumba madarasa 6 ambavyo vipo tayari huku akitoa rai kwa wananchi kuwa na mwamko wa kutoa michango ya shule waliyokubaliana kupitia vikao kwa lengo la kusaidia ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo.