WAZAZI na walezi wa wanafunzi katika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kutotumia kigezo cha serikali kutoa elimu bila malipo kuacha kuwahudumia watoto wao kwa mahitaji mengine wawapo shuleni.
Akizungumza na wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule ya Sekondari Sawe mwisho wa wiki; Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Julias Kakyama amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwahudumia watoto wao kwa mahitaji mbalimbali yaliyo nje ya ada.
Kakyama amewakumbusha wazazi na walezi kuwa bado wanao wajibu wa kuwahudumia watoto wao wakiwa shuleni kwa mahitaji ya chakula na sio kuwashindisha njaa kwa kisingizio cha kwamba serikali inatoa elimu bure.
Amesema kuwa serikali imeamua kutoa elimu bure lakini haijakataza wazazi au walezi kuwahudumia watoto wao mahitaji mengine kama vile sare za shule, chakula, ulinzi wa mtoto pamoja na kufuatilia maendeleo ya watoto wawapo shuleni.
Amefafanua kuwa wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha kuwa watoto wanapata chakula wawapo shule ili kuwawezesha kumudu vipindi vyote vya masomo darasani na kwamba kuwapatia watoto chakula kunasaidia kuzingatia masomo na kuongeza kiwango cha ufaulu.
“Katika mpango wa elimu bila malipo wazazi na walezi wajitahidi kutimiza wajibu wao wa kuwahudumia watoto huduma zile muhimu ikiwemo kuwanunulia madaftari, sare za shule na kuhakikisha kuwa wanapata chakula shuleni ”amesema Kakyama.
Amesema serikali ya awamu ya tano imefuta ada pamoja na michango mbalimbali iliyokuwa kero kwa wazazi na walezi ili kila mtoto wa kitanzania apate elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne bure, wawazi wanapaswa kuwahudumia watoto mahitaji mengine.
“Kwa sasa wazazi hamlipi tena ada wala michango; wajibu wenu ni kununua sare za shule na kununua mahitaji mengine kama kalamu, daftari na mabegi, Serikali inaendelea kuhamasisha mtimize wajibu kwa kuwanunulia watoto wenu sare hizo” ameongeza.
“Tunaomba mtimize wajibu wenu kuchangia chakula shuleni kwa sababu tunapotoa chakula shuleni tunapunguza utoro, tunaongeza umakini na ufuatiliaji kwa wanafunzi pale wanapofundishwa, wanafunzi wengi wao wanatoroka pale wanapohisi njaa na wakiondoka baadhi yao hawarudi” amesema afisa elimu huyo.
Hata hivyo Kakyama amehimiza wazazi kusimamia ipasavyo maadili ya watoto wao ili waweze kufanikiwa na kufikia malengo waliyojiwekea kitaaluma kwa kushirikiana na walimu katika kuhakikisha watoto wanakuwa na nidhamu ya kuridhirisha katika jamii inayowazunguka.
Pia amewataka walimu na wazazi kuhakikisha wanawasisitiza wanafunzi kutii sheria za shule ikiwemo uvaaji wa sare sahihi ya shule, kuheshimiana na kutumia lugha nzuri wanapowasiliana.
“Wazazi tuna jukumu kubwa la kusimamia suala la maadili ya watoto wetu, suala ambalo huwezi kulitenganisha na mafanikio bora kitaaluma kwani mtoto wenye nidhamu na maadili mema daima hufanya vizuri darasani na yule asiye na nidhamu huporomoka katika taaluma. Nasisitiza nidhamu na taaluma huenda pamoja, haiwezekani kuvitenganisha hata mara moja.” Amesisitizi Kakyama.
Akichangia kwenye mkutano huo mmoja wa wazazi waliohudhuria ameshukuru kwa kuelimishwa kuhusu nafasi ya mzazi katika kufanikisha elimu ya watoto wao akibainisha kuwa wazazi bado wanahitaji kuelimishwa na kukumbushwa mara kwa mara kuhusu mgawanyo wa majukumu hasa yanayowahusu wazazi katika elimu bila malipo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai