Gari Lasombwa na Mafuriko Wilayani Hai: Watatu Hawajulikani Walipo
Imetumwa: April 25th, 2021
Watu watatu hawajulikani walipo baada ya gari walilokuwa wakisafiria huko Kata ya Masama Mashariki Wilayani Hai kusombwa na maji walipo kuwa wakivuka daraja la mto Namwi.
Mmiliki wa gari hilo Bw.Curthbert Uroki amewataja waliokuwa ndani ya gari hilo kuwa ni Goodluck Ngowi,Joseph Uroki na Elia Lema.
Inadaiwa kuwa majira ya saa tatu usiku wakuamkia leo April 22 2021 walisikia mto Namwi ukiwa umefurika hali ambayo iliwafanya kuamka na baadhi ya wakazi wengine kuanza kuyakimbia makazi yao ili kunusuru maisha yao.
Mamia ya wananchi wa vijiji vya Sonu, Ngira na vijiji vilivyo pembezoni mwa mto Namwi wamesema kuwa hawajawahi shuhudia tukio hilo kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita.Majira ya saa tatu asubuhi lilionekana gari aina ya Toyota Hilux ambalo linadaiwa watu hao watatu walikuwemo ndani yake likiwa limefunikwa na vifusi na mchanga ambapo hadi majira ya saa kumi jioni jitihada za kulinasua gari hilo katika mto huo zilikuwa zikiendelea chini ya usimamizi wa kikosi maalumu cha zimamoto na uokoaji kwa kushirikiana na jeshi la akiba pamoja na wanachi.
Aidha Kamati ya ulinzi na Usalama wilaya ya Hai ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya, amesema kuwa bado wanafanya tathimini ya maafa hayo huku pia akisema wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari hasa wakati huu wa mvua.