Wanachama wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Hai Rural Teachers SACOSS wametakiwa kushirikiana na bodi mpya ya uongozi ili kufikia maendeleo yanayokusudiwa kwa chama hicho.
Akiongea baada ya kutangazwa mshindi wa kiti cha Mwenyekiti wa bodi hiyo Alex Warioba amewaomba wanachama kuendeleza utamaduni wa kushirikiana na viongozi katika kutekeleza majukumu ya chama.
“Mmekuwa karibu na uongozi unaomaliza muda wake na kushirikiana nao vizuri; ninaomba kwa niaba ya wajumbe wenzangu mtupe na sisi ushirikiano ili tuweze kutimiza malengo ya chama chetu” Amesema Warioba.
Uchaguzi uliofanyika kwenye viwanja vya CCM Sanya juu na kuhudhuriwa na zaidi ya wanachama 2000 umekipatia chama hicho uongozi mpya ambao utakuwa madarakani kwa muda wa miaka mitatu.
Alex Warioba amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa chama hicho na Anselm Hamaro akiibuka nafasi ya Makamu wa Mwenyekiti huku wajumbe wa bodi hiyo wakiwa William Temba, Richard Temba, Abdulbast Mohamed, Godfrey Kway na Justina Ngolinda.
Kamati ya usimamizi nayo imepata viongozi wapya kwa muhula wa miaka mitatu wakiwemo Hassan Mfangavo, Amani Perfect na Joshua Swai ambao kazi yao kuu itakuwa kusimamia utekelezaji wa kazi chama na kuhakikisha kuwa kazi zote zinafanyika kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo kwa muda wote watakapokuwa madarakani.
Naye Stanley Fundisha amechaguliwa kuwa mwakilishi wa wanachama kwenye shughuli zote zinazohusu maslahi ya wanachama akiwa kama jicho la wanachama wote kwenye utekelezaji wa kazi za kila siku za chama.
Hai Rural Teachers Saccos ni chama cha akiba na mikopo kinachohudumia watumishi wa umma katika wilaya za Hai na Siha kilichoanzishwa mwaka 2000 kikiwa na wanachama 67 waliokuwa viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya ya Hai kikiwa na mtaji wa shilingi 335,000 ambacho mwaka huu kikiwa kinatimiza miaka 21 na kwa ungozi Meneja wake Upendo Lyatuu akishirikiana na Bodi ya Uongozi chama kimefikisha wanachama 2,335 hadi mwisho wa mwaka 2020 na kinaendelea kuvutia wanachama wapya kupitia huduma bora zinazotolewa.
Chama hicho hadi kufikia 31/10/2020 kimeonesha ukuaji mkubwa ambapo akiba imeongezeka kutoka sh. 3,708,187,864 mwaka 2016 hadi kufikia 6,291,425,330 na kufanikiwa kutoa mikopo ya shilingi 41,513,612,000 tangu kianzishwe hadi mwisho wa mwezi Oktoba 2020 ambayo imewasaidia wanachama kufanikisha shughuli za kilimo, ufugaji, ujenzi wa nyumba za makazi na biashara, kununua vyombo vya usafiri na kuhudumia dharura mbalimbali ambazo wangefanikisha kwa shida nje ya chama hicho.