Halmashauri ya Hai Yamzawadia Mwanafunzi Kidato cha Sita
Imetumwa: September 29th, 2020
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai Yohana Sintoo amewataka walimu na wanafunzi katika wilaya hiyo kuthamini juhudi za Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa elimu nchini ikiwemo kutoa elimu bila malipo na kuboresha miundombinu ya shule.
Amesema Serikali inawekeza nguvu kubwa kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu ya uhakika huku wakiwa na vifaa vya kujifunzia kama vitabu na vifaa vya maabara pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya majengo ya vyumba vya madarasa, maabara na nyumba za walimu.
Sintoo ametoa kauli hiyo kwenye hafla ya kukabidhi zawadi kwa mwanafunzi Priscuss Joseph aliyefanikiwa kuingia kwenye orodha ya wanafunzi kumi waliofaulu vizuri kwenye mitihiani ya Kitaifa ya Kidato cha Sita iliyofanyika Juni 2020.
Sintoo amekabidhi cheti na shilingi laki tano za kitanzania kwa mhitimu huyo katika ukumbi wa halmashauri hiyo huku zoezi hilo la makabidhiano likishuhudiwa na waandishi wa habari, baadhi ya viongozi wa wilaya pamoja na walimu kutoka shule za sekondari na msingi wilayani humo.
"Sisi wilaya ya Hai tumejizatiti kuhakikisha kwamba elimu inafanya vizuri na dunia ijue kwamba tumekuwa tukifanya vizuri kwa mfululizo wa miaka minne (4) na miongoni mwa halmashauri mia moja themanini na sita (186) za Tanzania huwa tunachezea katika nafasi ya tano, sita, na saba ni mwaka huu tu ndio tumeshuka ingwaje sio sana" amesema Sintoo.
Kwa upande wake Priscuss baada ya kupokea zawadi amemshukuru Mkurugenzi pamoja na uongozi wa wilaya ya Hai kwa kumpatia zawadi hiyo kwani umeonyesha kumjali na kumpa heshima huku akiwaasa vijana wengine kuwaheshimu wazazi na viongozi wao kwani ndiko kwenye maarifa na baraka.
Uongozi wa wilaya ya Hai umesisitiza kwamba umejipanga kuhakikisha unajitahidi kukuza kiwango cha ufaulu kwa shule zote za wilaya yao kwa kuboresha miundombinu ya elimu pamoja kufuatilia shule zote kuhakikisha zinafanya vizuri katika ufundishaji kwani lengo la wilaya ya Hai ni kuwa kinara kitaifa.