Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hai Yohana Sintoo amewapongeza na kuwashukuru watumishi wa halmashauri hiyo kwa kuiwezesha halmashauri kupata hati safi.
Sintoo ametoa pongezi hizo katika kikao maalum cha baraza la madiwani na kusema kuwa uwajibikaji wa watumishi hasa katika ukusanyaji wa mapato na utoaji elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kulipa kodi ndicho kilichochangia kupata hati hiyo.
“Ni jambo la faraja kupokea taarifa nzuri; kwetu sisi kupata hati safi mfululizo miaka minne ni jambo la kujivunia na kipimo kwamba tunawajibika kwa sehemu yetu”, amesema Sintoo.
Aidha Sintoo amesema kuwa baada ya Halmashauri hiyo kupata hati safi, wataendelea kufanya kazi kwa weledi na bidii kuhakikisha kuwa halmashauri hiyo inaendelea kupata hati safi.
Kwa upande mwingine Sintoo amesema kuwa halmashauri yake imeanza kuweka na kutekeleza mpango madhubuti wa kuweka kipaumbele katika miradi ya kimkakati ikiwemo kulifanya soko la kwa Sadala kuwa soko la kimataifa.
Amesema mpango wa kufanya soko la Sadala kuwa la kimataifa unakusudia kujenga soko jipya na la kisasa kwenye eneo la halmashauri lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji huo.
Awali akizungumza na wanahabari nje ya ukumbi wa mikutano; Diwani wa Kata ya Machame Magharibi Martin Munisi amesema kuwa ujenzi wa soko hilo utasaidia kuondoa kero ambazo wananchi wanakutana nazo kwa sasa ikiwemo ndizi kuozea shambani au bidhaa kuuzwa kwa bei ndogo tofauti na thamani yake halisi.
Akizugumzia halmashauri kupata hati safi; Munisi amesema hii imetokana na watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi lakini pia kumekuwa na usimamizi mzuri wa rasilimali za umma huku vyote vikilenga kumhudumia mwananchi wa Wilaya ya Hai.
Kikao cha baraza la madiwani kimefanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Hai na kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo ya halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kupokea taarifa za utekelezaji wa kazi kwenye kazi ya kata.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai