Wito umetolewa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kutoa kiwango kikubwa cha fedha wanazowapa wanawake, vijana na wenye ulemavu ili kuwawezesha kutekeleza miradi yenye tija kwa jamii husika.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Kheri James kwenye mkutano wa ndani na wanachama wa chama hicho uliofanyika kwenye ukumbi wa Filomena wilayani Hai.
Amesema mikopo hiyo iangalie uwezekano wa wanaokopeshwa kutengeneza ajira za watu wengine ili kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira lakini pia kuwezesha wakopaji kutengeneza kipato cha kaya zao.
Aidha James ametumia mkutano huo kuwakumbusha vijana na wanachama wote wa Chama cha Mapinduzi kuwa wanao wajibu wa kutekeleza kwa chama na Taifa kwa ujumla hasa katika kipindi hiki ambapo nchi inapitia mabadiliko makubwa kwenye sekta zote kuelekea maendeleo endelevu.
“Leo hapa Hai nataka niwakumbushe umuhimu wa kuilinda nchi yetu, kuipenda nchi yetu na kuithamini nchi yetu. Nchi yetu ilipokuwa, ilipo na inapoelekea; kila mmoja anajua uelekeo wa nchi hii.”
“Ukishakuwa na miundombinu ya uhakika kwa anga, miundombinu ya uhakika kwa maji, miundombinu ya barabara; uchumi wetu utakuwa wapi baada ya leo”
Amewataka vijana kujiandaa kushiriki kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika miezi michache ijao kwa kupiga kura na kupigiwa kura kwa wale watakaogombea nafasi mbalimbali.
Kwa upande mwingine Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya amewakumbushwa wanachama kuwa hakuna kiongozi mwenye mgombe katika kinyang’anyiro cha kuwania uteuzi wa CCM kwa nafasi ya ubunge wa jimbo la Hai.
Nao Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro Ivan Moshi na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Hai Cedrick Pangani wamemwakikishia Mwenyekiti wa UVCCM Taifa kuwa wataendelea kushirikiana na vijana na makundi mengine kwenye jamii kuhakikisha kuwa chama chao kinapata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai