Kiongozi wa mbio za Mwenge 2018 Mhandisi Charles Kabeho amewataka madiwani kuacha itikadi za siasa katika kufanya maamuzi ya kugawa mikopo ya asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri inayotakiwa kutolewa kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akizungumza wakati wa mbio za Mwenge wilayani Hai Mhandisi Kabeho amesema lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa makundi yote maalum yanawezeshwa kiuchumi na inashangaza kuona baadhi ya madiwani wanatumia vibaya nafasi zao katika kukwamisha juhudi za serikali za kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi.
‘Fedha hizi ni kwa mujibu wa sheria na taratibu haijalishi kwamba halmshauri inaongozwa na nani au na chama kipi; cha msingi kanuni, taratibu na sheria ni lazima kuzingatiwa na halmashauri zote kwa kutenga fedha hizo na mara nyingi wakati wa mwenge tunagawa fedha hizi’ amesema Mhandisi Kabeho.
‘Nipende kuikumbusha Halmashauri inayoongozwa na Mh Mwenyekiti na Madiwani wake kwamba wakae tena na kuhakikisha kuwa wanagawa fedha hizo ili makundi haya muhimu yapatiwe mikopo ili waweze kujikwamua kichumi.’ amesisitiza Kabeho.
Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge ameagiza taratibu zingine zifuatwe endapo itaonekana ni vigumu kwa madiwani kuidhinisha fedha hizo za mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili vikundi vya ujasiriamali wilayani humo ambavyo vitakidhi vigezo viwezeshwe na kuendesha miradi yao kama ambavyo serikali imeagiza.
Awali akimkaribisha kiongozi wa mbio za mwenge Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya alisema Halmashauri imeshindwa kutoa mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwenye mapokezi ya Mwenge baada ya baadhi ya madiwani kugoma kupitisha mikopo hiyo kwasababu zisizo za msingi na kuhaidi kutumia taratibu zingine endapo Madiwani hao hawataidhinisha fedha hizo ili kuwasaidia wananchi wenye vigezo vya kupata mikopo hiyo na kwamba ndiyo sera ya serikali ya awamu ya tano ambayo yeye anaisimamia.
‘kama nilivyokuambia kiongozi wa Mbio za Mwenge na sasa nasema mbele ya Umma kwamba watu wachache wamekataa kuidhinisha fedha kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, nakuhakikishia kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kwamba hilo halitajirudia tena watu wachache kukaa na kuamua kuwa wengine waendelee kupata tabu wakati ule ni utaratibu wa kisheria, fedha zile ni za umma zinakusanywa kwa matumizi ya Umma, umma ni watu wanyonge na fedha hizo sio hisani.’alisema Sabaya
Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 umekimbizwa kwenye jumla ya kilometa 98 katika Wilaya ya Hai na kutembelea miradi ya maendeleo ambayo miradi miwili imezinduliwa na mmoja umewekewa jiwe la msingi yenye thamani ya shilingi milioni 461,649,943.
Miradi hiyo iligusa sekta ya kilimo kwa kuzindua shughuli za kusindika zao la vanilla, uzinduzi wa duka la dawa katika hospitali ya Wilaya ya Hai pamoja na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa ukuta wa uzio wa shule ya sekondari ya wasichana ya Machame.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai