Jamii Yatakiwa Kutunza Vyanzo vya Maji Bonde la Mto Pangani
Imetumwa: August 3rd, 2021
Wito umetolewa kwa jamii kutunza na kuhifadhi rasilimali maji pamoja na vyanzo vyake ili kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo huchangiwa kwa kiasi kikubwa na vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyotokana na shughuli za kibinadamu.
Akizungumza na wadau wa maji wa Bonde la Mto Pangani, madiwani wa halmshauri ya Hai wetendaji wa Kata na Vijiji pamoja na wenyeviti wao, Mkuu wa wilaya ya Hai Juma Irando amesema kuwa jukumu la kuhifadhi na kutunza vyanzo na rasilimali maji linapaswa kupewa uzito na jamii nzima na kufahamu kuwa ni jukumu la wote.
"Suala la maji ni mtambuka na linamgusa kila mmoja wetu, kwa mantiki hiyo bonde la Pangani na jumuiya zake zote peke yao haziwezi kuyatunza isipokuwa tunapaswa kutambua kuwa ni jukumu letu sote" amesema Irando.
Mbali na kutoa wito huo; Irando ameishauri bodi ya maji ya bonde la Pangani kutoa elimu ya utunzaji wa maji kwa kupanda miti ili kuboresha mazingira na kuepuka upungufu wa maji.
"Rasilimali maji ni ya kutunza sana maana ndio uhai wetu sote na kipekee niwashukuru ninyi bonde la Pangani kwa namna mnavyosimamia vyanzo vya maji ili vizidi kuwa endelevu lakini bado mnalo jukumu la kuhamasisha utunzaji wa mazingira yetu" Ameongeza.
Naye Mkurugenzi wa bodi ya Bonde la Pangani Segule Segule amesema kuwa bodi ya bonde hilo ipo kisheria na inafanya kazi katika mikoa mitatu ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga na kwamba ofisi yake inaendelea kutoa elimu kuhusiana na masuala yahusuyo rasilimali maji.
Amesema kuwa kutokana na elimu ambayo imekuwa ikitolewa baadhi ya wananchi wameanza kupata uelewa na kuanza kuchukua hatua muhimu katika kuhifadhi vyanzo vya maji.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Masama Kusini Cedric Pangani ameomba uongozi wa bonde hilo kuwashirikisha viongozi walioko katika jamii mipango waliyo nayo ili iweze kupata uungwaji mkono badala ya kuleta miongozo ambayo imekuwa ikioneonekana siyo shirikishi kwa wananchi ambao ndiyo wadau wakubwa katika utunzaji huo.
"Asitoke mtu juu na kuitisha mikutano huko kijijini kuelezea mambo ya vikundi vya Bonde la Pangani wakati Mtendaji wa kijiji, Mwenyekiti wa kijiji na hata Diwani hajui, Sisi ndiyo tulio na wananchi tushirikishwe ili tusaidiane nao na hii itaondoa ukakasi kwa jamii". Amesema Pangani.