Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro imefurahishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo unavyofanyika kwa ufanisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai
Akizungumza baada ya ziara ya kamati hiyo kutembelea miradi inayotekelezwa kwenye halmashauri hiyo; Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania Mkoa wa Kilimanjaro na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa huo Zuhura Chikira amesema amefurahi kuona matumizi mazuri ya fedha za Serikali katika kutekeleza miradi.
“Nimeona kazi nzuri inayofanywa na kila mmoja kwa nafasi yake; Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na wataalamu wake bila kusahau chama”
“Binafsi nimeridhika kwa ufanisi niliouona hasa matumizi sahihi ya fedha za Serikali kutekeleza miradi inayoonekana yenye ubora na kuonesha thamani halisi ya fedha zilizotumika. Nitafikisha salamu zenu kwa chama chetu ngazi ya Mkoa hadi ngazi ya Taifa” amesema Chikira.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa anayetokea Wilaya ya Hai Yassin Lema pamoja na kupongeza mafanikio ya utekelezaji wa miradi amewakumbusha viongozi wa chama na serikali kuendelea kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo ili kuongeza kasi ya maendeleo.
“Viongozi wa chama na halmashauri waendelee kuelimisha wananchi umuhimu wa kuchangia shughuli za maendeleo hasa ikizingatiwa tulikotoka kuna wenzetu waliwaambia wananchi kuwa serikali inafanya kila kitu hivyo kupunguza ushiriki wa wananchi” Amesisitiza Lema.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Hai ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo na Diwani wa Kata ya Muungano Edwin Rutaraka ameonesha kuridhishwa na hali ya utekelezaji wa miradi hasa kwenye matumizi mazuri ya fedha za Serikali.
“Tumepokea maelekezo yaliyotolewa, kwa sehemu yetu kama chama tutaisimamia Serikali kuona wanatekeleza kama ilivyoelekezwa kwa ufanisi” Amesema Rutaraka.
Akizungumza kwa niaba ya wataalamu wa serikali; Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo ameishukuru kamati ya siasa mkoa kwa kutembelea miradi katika halmashauri yake na kwamba maagizo yaliyotolewa yatafanyiwa kazi kwa ufanisi ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Aidha Sintoo amebainisha kuwa anafarijika kufanya kazi na Chama cha Mapinduzi kutokana na umakini uliopo kupitia mfumo wa chama hicho na kuahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa chama katika kuhudumia wananchi.
“Tunaomba wenzetu wa chama na viongozi waliopo kwenye jamii kuhamasisha wananchi kuanzisha miradi. Sisi kama halmashauri tutaendelea kufanya ukamilishaji kwa miradi inayoanzishwa na jamii; wakijenga boma sisi tutaleta vifaa vya kupaua” Amesisitiza Sintoo.
Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro imekagua mradi wa kukarabati shule kongwe za Sekondari ya Lyamungo Sh. 799,443,156, Sekondari ya Wasichana Machame wa Sh. 847,658,579.
Pia kamati hiyo imekagua miradi ya kwenye shule za msingi ikiwemo ujenzi wa chumba kimoja cha darasa Shule ya Msingi Narumu Tella kinachotekelezwa kwa nguvu ya wananchi kwa Sh. 1,187,000. Ujenzi wa vyumba 4 vya madarasa na matundu 5 ya choo kwenye shule ya Msingi Kibaoni unaogharimu Sh. 85,500,000 pamoja na ujenzi wenye thamani ya Sh. 240,413,000 wa vyumba 7 vya madarasa na matundu 8 ya vyoo kwenye shule ya Msingi Kibohehe ambapo Ubalozi wa Japan umechangia Sh. 206,000,000 na nyingine kutoka halmashauri na wadau mbalimbali.
Halmashauri ya Wilaya ya Hai imejizatiti kufanya ukarabati wa mara kwa mara wa shule zake za msingi ili kuziweka kwenye mazingira bora ya kufundisha na kujifunzia na hatimaye kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai