Katibu Tawala Wilaya Wella Awakumbusha Wauguzi Kuwajali Wagonjwa
Imetumwa: May 11th, 2021
Wauguzi nchini wametakiwa kuimarisha utendaji wao kwa kufanya kazi kwa bidii, kujitoa na kuwajali wagonjwa wanaowahudumia ili kuepuka kuhatarisha maisha ya wananchi kutokana na uzembe wa baadhi yao.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Hai Upendo Wella wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya siku mbili ya Siku ya Wauguzi Duniani katika viwanja vya Snow View kwenye Kata ya Bomang’ombe.
Wella amewataka wauguzi kutumia taaluma zao katika kuhakikisha kuwa wanatoa huduma iliyo bora kwa kuzingatia uadilifu wa kazi yao na kuongeza umakini ili kuleta matokea mazuri kwa wanaowahudumia.
Kwa upande mwingine pia Wella amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo ili kupata nafasi ya kupima na kujua afya zao kwani kuna umuhimu wa kufanya hivyo na vipimo hivyo ni bure.
Mbali na hayo Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Gaudencia Ulomi amesema hawatasita kumchukulia hatua mtumishi wa afya ambaye hatafuata maadili ya kazi yake huku akisisitiza kuwa wauguzi ni watu muhimu sana na wamepewa heshima ya kuangalia afya za watu hivyo wanapaswa kuwa makini.
Aidha Ulomi amesema kuwa Mkoa wa Kilimanjaro ndiyo wa kwanza kuunda kamati ya nidhamu kwa watumishi wa kada ya afya ikilenga kuondoa malalamiko yanayojitokeza kwa baadhi ya wauguzi na watu wengine wa kada ya afya.
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani kitakuwa ni tarehe 14 Mei 2021 ambapo kimkoa yatafanyika katika Wilaya ya Hai kwenye Uwanja wa mpira wa CCM Bomang’ombe na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira.