“Tunaishukuru sana serikali kwa hatua hii, ni kitu ambacho hatukutegemea kwani tangu mwaka 1996 mimi mwenyewe nafuatilia suala hili na hatukuwahi kupata suluhu, namshukuru sana Rais John Pombe Magufuli pamoja na serikali yote”
Hii ni kauli ya Saidi Omari miongoni mwa wananchi waliohudhuria kikao kilichofanyika leo kati ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi na wananchi wa kijiji cha Nshara pamoja na bodi ya mradi wa umoja wa vyama vitatu vya ushirika vya Foo, Nronga na Wari katika shamba la Lambo Estate.
Katika kikao hicho Waziri Lukuvi ameagiza kaya 78 za wananchi waliokuwa wafanyakazi wa mashamba ya mkonge (Lambo Estate) wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro kupewa ekari 156 ikiwa ni utatuzi wa mgogoro kati ya wananchi hao na mradi wa umoja wa vyama hivyo.
Agizo hilo limekuja baada ya mgogoro wa shamba la Lambo Estate na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Nshara ulionza tangu miaka ya tisini baada ya wanachi hao kutuma maombi serikalini wakiomba kupewa eneo la makazi ikifuatiwa na tukio la ajira yao kukoma ambapo mwaka 2001 wafanyakazi hao walifungua kesi kwa kutoridhika na stahiki walizolipwa na mradi huo.
Mwaka 2003 Mahakama iliamuru wafanyakazi hao waendelee kuishi kwenye nyumba za ushirika na wapewe hekari 50 kwa ajili ya kuwawezesha kufanya shughuli za kilimo pasipo kujenga makazi ya kudumu.
Akizungumza na wananchi pamoja menejimenti ya bodi ya vyama hivyo Waziri Lukuvi amesema serikali ya Awamu ya Tano haiwezi kuona wanyonge wakiendelea kuteseka kwa sababu ya watu wachache na kwa sababu hiyo imeagiza wananchi hao wasifukuzwe katika eneo hilo.
“Hamuwezi kujikusanya huko wajanja wachache na kutaifisha ardhi za vijiji alafu mnawakodisha wananchi ardhi na kutumia fedha hizo, huu ni ukoloni kabisa safari hii tutanyoosha maneno yote haya yaliyopinda kwani serikali hii ya awamu ya tano haitacha mambo haya yapite hivi” amesisitiza Lukuvi.
Kufuatia hatua hiyo amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya kusimamia zoezi la upimaji wa ardhi hiyo ili kuziwezesha kaya hizo kupata hekari 2 kwa ajili ya makazi na shughuli za kilimo na uzalishaji wa chakula kwa masharti ya kutouza maeneo watakayopewa.
Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi ameuagiza uongozi wa NDC kulipa kabla ya mwezi Disemba kodi ya ardhi ya eneo wanaolimiki na kufanyia kazi tangu walipokabidhiwa eneo hilo ili kuwawezesha kupewa hati miliki ya eneo hilo na endapo hawataweza kufanya hivyo taratibu za kulirudisha eneo hilo kwa serikali.
Akizungumza katika eneo hilo la machine tools ameagiza wananchi wote waliomilikishwa maeneo katika eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 1000 na wameshindwa kuliendeleza wapewe notisi ya siku tisini ili taratibu za kuchukua eneo hilo na kwa wale waliopimiwa na hawana hati ya umiliki orodha yake ifikishwe kwake na wapewe taarifa ya kutokuwa na umiliki wa eneo hilo.
“Asiye na hati niorodhesheni tu nitatoa idhini ili tutangaze watanzania wengine na wawekezaji wageni wenye uwezo wa kuwekeza waje wawekeze, eneo hili limekaa muda mrefu pasipo kuendelezwa na lipo mjini”
Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya amemweleza Waziri kuwa amepokea maagizo yote yaliyotolewa kwenye ziara hiyo na kuweka bayana kuwa atayatekeleza kwa nguvu zote ili haki ya kila mhusika ipatikane lakini pia kuiwezesha serikali kukusanya mapato stahiki kutokana na kodi zitakazolipwa kwenye maeneo hayo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai