Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Juma Irando ametoa agizo kwa meneja wa Tanesco wilayani humo kuhakikisha umeme unawaka katika shule ya sekondari Lyasikika kufuatia shule hiyo kukosa umeme kwa zaidi ya miaka 10.
DC Irando ametoa agizo hilo leo Agosti 12, 2021 alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Lyamungo kati Kata ya Machame Mashariki katika mkutano wa hadhara unaoendeleza ziara zake katika kata za wilaya hiyo kwa lengo la kujitambulisha, kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
"Taasisi zote za Serikali zinatakiwa zipate umeme ikiwa ni pamoja na hiyo shule. Tanesco ninawaagiza kufikisha umeme kwenye shule hiyo". Amesema Irando.
Kwa upande wake meneja wa Tanesco wilaya ya Hai Daniel Kyando ameahidi kuwa atahakikisha ndani ya miezi mitatu shirika hilo litakuwa limewasha umeme katika shule hiyo ili kuondoa adha ya kukosekana kwa nishati hiyo.
Naye mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hai Dionis Muyinga amewataka viongozi wa taasisi zote za serikali kuhakikisha wanafunga nyaya kwenye taasisi hizo ili iwe rahisi kwa Tanesco kuunganisha umeme kwa haraka.